Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amesema hii leo kwamba, ana nia ya dhati ya kukabidhi madaraka kwa mrithi atakayechaguliwa wakati ambapo wito wa kuundwa kwa serikali ya mpito ukiendelea kutolewa. Ghani ameyasema hayo katika kipindi cha mahojiano na kituo cha utangazaji cha CNN.
Wiki iliyopita mwanachama wa timu ya mazungumzo ya Afghanistan Hafiz Mansour alisema kwamba, baadhi ya nchi ziko tayari kuisaidia Afghanistan kuanzisha serikali ya mpito ambayo itapisha njia kuundwa Serikali mpya. Wawakilishi wa serikali ya Afghanistan tayari wamewasili Doha na watakuwa na kikao cha kwanza na wawakilishi wa Taliban leo.
Wakati juhudi hizo zikiendelea kundi la Taliban limemuua mke wa askari katika jimbo la kaskazini la Sar-e Pul na makabiliano mengine yametokea katika jimbo jingine la Takhar na kuwaua askari watano na wengine watano kujeruhiwa.
