Mawakili wa Navalny kukata rufaa uamuzi wa kufungwa jela


Mahakama nchini Urusi inatarajiwa kutoa leo uamuzi wa kesi ya rufaa ya kupinga kifungo cha siku 30 dhidi ya mkosoaji wa serikali Alexei Navalny kabla ya kuanza kesi yake. 

Mawakili wa Navalny wanatumai kuwa mahakama ya Khimki karibu na mji mkuu Moscow itamuachilia huru mwanaharakati huyo mwenye umri wa miaka 44.

 Anatuhumiwa na waendesha mashitaka wa Urusi kwa kukiuka adhabu ya awali ya kifungo kilichoahirishwa kwa kwenda nchini Ujerumani. Timu ya Navalny imeitisha maandamano Jumapili ijayo bila kujali uamuzi wa leo wa mahakama. 

Maafisa wa polisi mjini Moscow wamefanya uvamizi na kuendesha upekuzi mkali kwenye majengo na ofisi zenye mafungamano na familia au washirika wa Navalny pamoja na kumkamata kaka yake. 

Aidha, wapelelezi wamesema leo kuwa wamefungua kesi ya uhalifu dhidi ya Leonid Volkov, mshirika wa karibu wa Navalny, wakimtuhumu kwa kuwahimiza vijana wadogo kushiriki katika maandamano haramu.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi