Timu ya watalaamu wa Shirika la Afya Duniani - WHO imeondoka leo kwenye karantini katika mji wa Wuhan nchini China ili kuanza uchunguzi wake wa vyanzo vya virusi vilivyosababisha janga la ugonjwa wa COVID-19.
Watafiti hao, ambao walihitajika kuwa kwenye karantini kwa siku 14 baada ya kuwasili China, wameondoka leo hotelini walimokuwa na haikubainika haraka walikoelekea.
Ujumbe huo wa watalaamu umegubikwa na siasa, huku China ikilenga kujiondolea lawama kwa tuhuma za kutochukua hatua za mapema kuhusiana na mripuko wa virusi vya corona.
Swali muhimu ni upande gani wa China utakaowaruhusu watafiti hao kwenda na wataweza kuzungumza na nani.
Mapema mwezi huu, afisa wa zamani wa WHO Keiji Fukuda, ambaye siyo sehemu ya ujumbe ulioko Wuhan, alitahadharisha dhidi ya kutarajia mafanikio yoyote, akisema inaweza kuchukuwa miaka kabla ya kufanya mahitimisho yoyote thabiti kuhusu chimbuko la virusi hivyo.
