Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ameipandisha hadhi halmashauri ya Wilaya ya Kahama Mji kuwa Manispaa ambapo sasa Kahama Mji itajulikana kama Manispaa ya Kahama akisema wilaya hiyo imemfurahisha kwa kuwa na mipango mikubwa anayoitaka ikiwa ni pamoja na kufanya kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa fedha zake za ndani.
Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamis Januari 28,2021 wakati akizungumza na wananchi katika uwanja wa taifa wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambapo wananchi waliokuwa katika mkutano huo walishangilia kutokana na tangazo hilo.
“Nimeshangaa kweli, kwamba wilaya hii ya Kahama ina mipango mikubwa ninayoipenda. Na mimi nasema kwa sababu mmenipa kura halafu mimi ndiyo Rais na kazi ya kupandisha ninyi mmenipa, ninaipandisha iwe manispaa, na hiyo hospitali ya Kahama iwe na hadhi ya Manispaa na nitahakikisha mji wa Kahama unajengewa barabara za lami ili ziendane na hadhi ya manispaa”, amesema Rais Magufuli.
“Nina sababu za msingi za kuipandisha, kwanza mapato ya wilaya ya Kahama katika mkoa mzima wanachangia asilimia 50, hata makusanyo ya mapato ni miongoni mwa halmashauri zinazoongoza kwa makusanyo. Hata kura mlinipa kwa wingi, hata katika miradi ninyi mnajitegemea,” amesema Rais Magufuli.
“Najua kule Shinyanga hawana raha, lakini kikubwa mimi ninataka maendeleo na watu wanaoamua kutengeneza maendeleo yao, mimi lazima niwaunge mkono. kwa hiyo Kahama mmenigusa sana”,ameongeza.
Mkoa wa Shinyanga sasa utakuwa na Manispaa mbili (Manispaa ya Shinyanga na Manispaa ya Kahama), lakini pia kuwa na halmashauri za wilaya nne ambazo ni halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Shinyanga, Ushetu na Msalala.
