Wiki moja baada ya kuingia madarakani, Rais wa Marekani Joe Biden ametuma onyo la wazi kwa China dhidi ya nia yake ya kutaka kujitanua katika kanda ya Asia na Kusini Mashariki mwa Asia.
Katika wito alioutoa pamoja na taarifa kadhaa, Biden na maafisa wake waandamizi wa usalama, wamesisitiza uungwaji mkono kwa washirika wao Japan, Korea Kusini, Taiwan na Ufilipino, wakiashiria kupinga madai ya China ya umiliki wa maeneo hayo yanayogombaniwa.
Biden amemwambia Waziri Mkuu wa Japan Yoshihide Suga kuwa utawala wake umedhamiria kuilinda Japan, vikiwemo visiwa vya Senkaku, ambavyo vinagombaniwa na Japan na China, ambayo inaviita Visiwa vya Diaoyu.
Msimamo huo umesisitizwa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, aliyemwambia mwenzake wa Japan Nobuo Kishi kuwa visiwa hivyo vinavyogombaniwa vipo kwenye Mkataba wa Usalama kati ya Marekani na Japan.
