Hyasintha Ntuyeko alikuwa akipata maumivu makali ya tumbo kila anapokuwa kwenye siku zake. Hali hiyo ilimtesa na akaamua kutafuta suluhu ya kudumu.
Alianza kama mfanyabiashara baadaye akageuka kuwa mzalishaji wa taulo za kike zenye mkaa wa mianzi ambayo husaidia kupambana na bakteria, fangasi na vijidudu vingine vinavyosababisha harufu mbaya, mwasho au maambukizo ya ugonjwa sehemu hizo.
Akiwa na mtaji wa Sh60,000 Hyasintha alianza biashara ya kuzifuata taulo hizo nchini Kenya kisha kuja kuziuza Tanzania. Aliisimamia vyema biashara hiyo ambayo sasa mtaji wake ni zaidi ya Sh20 milioni. “Nilianza ujasiriamali nikiwa na umri wa miaka 24, kulikuwa na changamoto nyingi. Familia yangu na marafiki hawakuamini kama naweza kusimama, ilibidi nifanye bidii kujenga uaminifu,” anasema.
Ingawa wengi wanaomzunguka waliuona ugumu wa mafanikio kutokana na maji mdogo aliokuwa nao, Hyasintha haamini katika kuanza biashara na fedha nyingi kwani kwa miaka 11 aliyodumu kwenye biashara hiyo, mambo mengi yamebadilika.
Hyasintha alianza biashara hiyo baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph alikopata shahada ya mifumo ya habari na uhandisi mitambo. Kisha alifungua kampuni ya Kasole Secrets ambayo sasa inatengeneza taulo hizo zinazosambazwa katika nchi kadhaa Afrika.
Wazo la kutengeneza taulo hizo za kike anazoziita Glory Pads zenye mkaa wa mianzi alilipata miaka saba iliyopita baada ya msambazaji wa jumla nchini Kenya, alikokuwa anazichukua kufunga biashara.
