Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amebainisha mambo 10 ambayo serikali yake imeyafanya ndani ya siku 100 tangu alipochaguliwa kuongoza visiwa hivyo katika uchaguzi wa Oktoba 28.
Dk Mwinyi alibainisha hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali ambayo serikali yake imeyafanya tangu alipochaguliwa na wananchi na kuunda serikali.
Jambo la kwanza, alisema mara baada ya kuingia madarakani alianzisha maridhiano na umoja wa kitaifa akitambua kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.
“Nilipoingia madarakani, nilitambua fika kwamba hatuwezi kuleta maendeleo kama hatuna mambo makuu ya msingi; la kwanza ni amani na la pili ni umoja wa wananchi wetu,” alisema Rais Mwinyi.
Alisema baada ya maridhiano aliunda serikali kwa kuteua baraza la mawaziri na makatibu wakuu. Alisema amepunguza ukubwa wa serikali ili fedha nyingi zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo.
Alisema katika uteuzi wake amezingatia masuala muhimu kama vile jinsia, uwajibikaji, makundi maalumu na uwakilishi wa mikoa.
Suala jinsine alisema ni kusimamia uchumi wa bluu kama msingi mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambapo wamezungumza na wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji katika bandari za Bumbwini na Mangapwani.
“Wenzetu wa Oman wako tayari kushirikiana na sisi katika hili na kama mlivyoshuhudia, tulishatia saini makubaliano ya awali,” alisema Rais Mwinyi na kusisitiza kwamba wamefanya pia mazungumzo ya uendelezaji wa bandari ya Mpigaduri.
Kiongozi huyo alitaja eneo la moundombinu kama jambo jingine ambalo wamelifanyia kazi ndani ya siku 100 ambapo alifanya mabadiliko kwa kuweka uongozi mpya na sasa matokeo yameanza
Alisema mapato katika bandari ya Malindi yameongezeka kutoka Sh4.3 bilioni kwa mwaka mmoja uliopita lakini kwa Disemba peke yake iliingiza faida ya Sh2.1 bilioni.
“Imeonekana wazi kwamba mapato yaliyopatikana Desemba ni sawa na mapato ya miezi sita. Tumeanza kupiga hatua nzuri ya ukusanyaji wa mapato,” alisema Rais Mwinyi.
Mbali na hatua hizo, alisema aliamua kufanya mikutano na wadau muhimu ambapo tangu ameingia madarakani amekutana na wafanyabiashara, wadau wa afya na elimu kwa lengo la kutambua changamoto zao.
Alizungumzia pia suala la uwajibikaji ambapo serikali yake imelisimamia kikamilifu na tayari watumishi wa umma wameanza kuzingatia maelekezo yake ya kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika sehemu yake ya kazi.
“Nafurahi kusema wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, maofisa ardhi, wamebeba maagizo yangu ya kuwahudumia wananchi na kuhakikisha kwamba matatizo ya ardhi yanapatiwa ufumbuzi,” alisema.
Maeneo mengine ambayo serikali yake imeyafanyia kazi ni utawala bora, ushirikiano na sekta binafsi pamoja na kupambana na udalilishaji wa kijinsia unaofanywa katika visiwa hivyo hasa dhidi ya wanawake.
“Tumewasimamisha zaidi ya wafanyakazi 80 ambao aidha walikuwa wanacheza na mitandao ile ya mapato ya serikali na wengine wamethibitika wanakula rushwa,” alisema Rais Mwinyi wakati akizungumzia utawala bora
