Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis, amelaani tukio la wiki iliyopita la wanafunzi wa kike zaidi ya 300 kutekwa nyara nchini Nigeria na kukiita kitendo hicho kama kitendo kisichokubalika.
Katika hotuba yake ya kila wiki katika uwanja wa mtakatifu Petro mjini Vatican, Papa Francis amesema anaungana na maaskofu wa Nigeria kulaani kitendo hicho huku akitoa wito wa maombi kwa wanafunzi hao ili warejee nyumbani haraka.
Wanafunzi wengine kadhaa hawajulikani waliko baada ya watu waliojihami kulishambulia bweni la shule moja siku ya Ijumaa Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.
Magenge ya uhalifu yameimarisha mashambulizi yao katika eneo hilo na katikati mwa Nigeria wakiwateka nyara wanafunzi kwa nia ya kupata fidia, kuwabaka na kuwaibia.
Wapiganaji wa kiislamu wenye itikadi kali kaskazini Mashariki mwa taifa hilo la Afrika awali waliishitua dunia kwa kuwakamata wanafunzi kadhaa kama sehemu ya kuonesha kutoridhishwa kwao au kupinga elimu ya Magharibi katika eneo hilo.
