Serikali Haiti yadai kutibua njama ya mapinduzi

 


Serikali nchini Haiti imesema jana kwamba wametibua njama ya mauaji dhidi ya rais Jovene Moise na kuipindua serikali, mnamo wakati mzozo ukizidi juu ya lini muhula wake unamalizika. 


Kwa mujibu wa waziri wa sheria Rockefeller Vincent, njama hiyo ilikuwa jaribio la mapinduzi, na mamlaka zimewatia mbaroni watu wasiopungua 23, akiwemo jaji mwandamizi na afisa kutoka polisi ya taifa. ''Jaji alikamatwa. Alikutwa huko chini ya masaa 48 huko Flagrante delicto. Amekamatwa pamoja na inspekata Jenerali wa polisi. 


Walikuwa wanapanga kumtia mbaroni rais na kumpeleka Petit Bois. Na walipanga kuvamia ikulu ili kumuweka rais wa muda ambaye tayari alikuwa ameandaa hotuba.'' 


Wanasiasa wa upinzani wametupilia mbali madai ya jaribio la mapinduzi, na kusema rais Moise hangeweza kupinduliwa kwa sababu muhula wake wa urais ulikuwa umeisha, na habari za hivi punde zinasema vyama vya upinzani vimemteua Jaji Joseph Mecene Jean-Louis, mwenye umri wa miaka 72 kuwa kiongozi wa muda.


Moise amekuwa akitawala bila udhibiti wa madaraka yake kwa muda wa mwaka mmoja uliopita, na anasema anabakia kuwa rais hadi Februari 7, 2022, katika tafsiri ya katiba iliyokataliwa na upinzani ulioongoza maandamano kusisitiza kuwa muhula wake uliisha jana.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi