Mkuu wa shirika la afya duniani Tedros Adhanon Ghebreyesus leo ameikaribisha hatua ya Marekani ya kujiunga katika mpango unaoungwa mkono na WHO wa kuimarisha juhudi za kupambana na Covid-19.
Hatua ya Marekani imechukuliwa na rais mpya wa nchi hiyo Joe Biden baada ya kuubadili mwelekeo uliochukuliwa na utawala wa zamani wa Donald Trump.
Mpango huo wa WHO wa juhudi za kupambana na Covid-19 unaojulikana kama ACT unahusisha uchangishaji fedha za kutengeneza chanjo, upimaji pamoja na usimamizi wa matibabu ili kulimaliza janga hilo.
Hata hivyo hadi sasa mpango huo unakabiliwa na upungufu wa kiasi dola bilioni 27 kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu huyo wa WHO Ghebreyesus.
Amesema uamuzi wa Marekani wa kujiunga na juhudi hizo ni muhimu huku pia akisisitiza kwamba ushirikiano wa kimataifa unazidi kupungua na kusababisha janga hilo kuongezeka licha ya chanjo kadhaa mpya kuidhinishwa.
