Wananchi watakiwa kujitokeza katika mbio za mwenge wa uhuru


Na Thabit Madai,Zanzibar.

WANANCHI wa Mkoa wa Kusini Unguja wametakiwa kuwa tayari na kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa kitaifa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021 ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 17 mei katika Uwanja  wa Mwehe Makunduchi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Tunguu, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid amesema kuwa Mkoa wa Kusini unguja umepata fursa ya kuwa wenyeji wa uzinduzi wa mbio hizo, hivyo wanatakiwa kujitokeza kwa wingi na kuweka historia ya mkoa huo.

“Ofisi ya Mkoa wa Kusini Unguja imepokea barua kutoka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwenge wa Uhuru utazinduliwa rasmi tarehe 17 mei katika viwanja vya Mwehe, Mkunduchi,” Alisema.

Alieleza  kuwa taratibu za maandalizi zinaendelea na tayari zimefikia katika hatua ya kuridhisha kukamilisha maandalizi hayo.

“Maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge umekamilika kwa kutayarisha kiwanja  ambacho kitafanyika uzinduzi huo pamoja na kufikisha huduma ya maji, umeme na vyoo ambapo huduma hizo zinatarajiwa kukamika ndani ya mwezi huu”, alieleza

Hata hivyo alifahamisha kuwa katika Mbio hizo miradi mbalimbali itazinduliwa, itatembelewa na kuweka mawe ya msingi.

 Aidha Mkuu wa Mkoa amefahamisha kuwa lengo la kutembeza mwenge  nchini ni kushiriki kwa pamoja katika kuleta Maendeleo bila ya kubagua itikadi ya  chama cha siasa  , rangi, kabila au dini  hivyo kila mwananchi ni wajibu kushiriki katika uzinduzi huo.

Hata hivyo aliwataka wananchi kushirikiana kushiriki katika uzinduzi wa huo ili kuweza kufanikisha kwa lengo la kuleta maendeleo nchini.

Mwenge huo wa uhuru utakimbizwa katika mkoa wa Kusini kwa muda wa siku mbili,tarehe 17 na  18  na baadae kukabidhiwa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuendelea na mbio zake

Mwenge huo wa uhuru mwaka huu umebeba kauli mbiu, TEHAMA NI MSINGI WA TAIFA ENDELEVU; ITUMIE KWA USAHIHI NA UWAJIBIKAJI.

 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi