Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuhakikisha linawasaidia Wazee kufanya shughuli nyingine za kiuchumi kufutia kutangaza hadharani kuacha ujangili na kusalimisha baadhi ya mfano wa silaha za jadi walizokuwa wakizitumia kuua Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Hatua hiyo ya kukabidhi silaha hizo imekuja kufutia TANAPA kuchangia kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga Zahanati ambayo imekamilika na imeanza kuwahudumia Wananchi wa Kijiji hicho ambapo hadi sasa jumla ya Wanawake wajawazito 19 wamejifungua salama.
Ametoa agizo hilo leo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kihumbu kilichopo katika wilaya ya Bunda mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara
Dkt. Ndumbaro amesema kitendo kilichofanywa na Wazee hao kutangaza hadhrani kuachana na uwindani haramu ni jambo la kupongezwa na kila Mtanzania mwenye kupenda shughuli za Uhifadhi nchini.
Kufuati hali hiyo Waziri Dkt. Ndumbaro ametaka Wazee hao kutafutiwa Shughuli nyingine za kiuchumi ambazo ni rafiki kwa uhifadhi ikiwamo ufugaji nyuki.
”Wazee hawa wapeni Mizinga ya nyuki kwa idadi watakayohitaji waweze kufuga nyuki” amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Aidha, Dkt. Ndumbaro amewashukuru Wazee hao kwa kuonesha mfano bora kwa vijana kuwa Wanyamapori waliopo katika Hifadhi ya Serengeti ni kwa ajili yao na Watanzania wote.
”Wazee wangu nawashukuru sana leo ni siku ya kihistoria katika Kijiji hiki, KItendo cha kukabidhi silaha hizi ni jambo la kuigwa na jamii yote na mumeonesha uelewa mkubwa katika masuala ya Uhifadhi nchini” alisema Dkt. Ndumbaro
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wazee aliyekabidhi silaha hizo, Joseph Mrisho amesema wao kama Wazee wamesukumwa kukusanya na kusalimisha silaha hizo kutokana na TANAPA inavyowachangia katika shughuli zao za Kimaendeleo
Amesema Zahanati hiyo iliyojengwa kwa msaada mkubwa wa fedha kutoka TANAPA umewaadhihirishia Wazee kuwa Wanyamapori ni fedha hivyo hawatakiwi kuwindwa kwa ajili ya Kitoweo.
Kwa Upande wake Mwakilishi wa Wazee kwa upande wa Wanawake, Suzan Magori amesema tangu Zahanati hiyo kukamilika jumla ya akina Mama Wajawazito wameweza kujifungua salama katika Zahanati hiyo ilhali hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma hiyo
” Sisi wanawake tunaishukuru sana TANAPA kwa kutupunguzia adha tuliyokuwa tukiipata hapo awali tunaamini ahata vifo vya akina Wanawake watakaokuwa wakijifungua katika Kijiji hiki kupitia Zahanati hii vitapungua.



