WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema katika mwaka 2020, jumla ya ajali za bodaboda na bajaji zilikuwa 404 ambazo zimesababisha jumla ya vifo 281 huku wengine 320 wakijeruhiwa.
Simbachawene ametoa takwimu hizo leo (Jumanne) katika Mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na Vijana uliofanyika katika viwanja vya Nyamagana, jijini Mwanza.
Amebainisha kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi kupitia kitengo chake cha Usalama Barabarani, bado taifa linapoteza vijana wengi kwa vifo na kusabibisha upotevu wa nguvu kazi pamoja na hali ngumu kwa wategemezi hususani watoto na wazazi wao.
Aidha, amewaonya waendesha bodaboda na bajaji kutotumia kigezo cha kushushiwa kiwango cha tozo ya adhabu kutoka Shilingi 30,000 hadi Shilingi 10,000 kama nafasi ya kuvunja sheria ya Usalama Barabarani.
