Jeshi la Polisi latakiwa kushirikiana na wananchi


Na Thabit Madai, Zanzibar

NAIBU Waziri Mambo ya Ndani Khamis Hamza Chilo amelitaka Jeshi la Polisi Wilaya ya Kati kushirikiana na Wananchi wa Shehia ya Tunduni katika kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya katika Shehia hiyo.

 

Akizungumza na wananchi  wa Tunduni Mkoa wa Kusini Unguja, katika muendelezo wa ziara yake ya kutembelea wananchi wa Jimbo la Uzini, alisema ipo haja ya kuhakikisha changamoto zote za Wananchi zinapatiwa ufumbuzi.

 

Amesema Shehia ya Tunduni, inakabiliwa na changamoto ya uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya jambo ambalo limekithiri na kusababisha vijana wengi kujiingiza katika vitendo viovu.

 Alieleza kuwa, vijana wamekuwa wakijiingiza katika vitendo vya Ulevi, Wizi wa mazao na mifugo pamoja na vitendo vya Udhalilishaji mambo ambayo huwakosesha amani wananchi wa Kijiji cha Tunduni na Vijiji jirani.

 

Amesema kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni jambo lisilo kubalika , hivyo ni lazima Jamii ishirikiane na Jeshi la Polisi  katika kupiga vita dawa za kulevya nchini.

 

“Ni lazima tuondoshe  muhali ndani ya Jamii, wauzaji wa dawa za kulevya tunawajua , ni ndugu zetu, watoto wetu, au marafiki zetu wa karibu, hivyo tushirikiane ili tuweze kumaliza tatizo hili.” Alisema Mbunge huyo.

 

Amesema kuwepo kwa ulinzi shirikishi wa shehia na kwa kushirikiana na jeshi la polisi itasaidia katika kutokomeza tatizo hilo.

 

Aidha ameeleza ipo haja kuiangalia upya  sheria ili wauzaji wa dawa za kulevya  wanapokamatwa wasipatiwe dhamana kama ilivyo kwa kesi za udhalilishaji.

 

Chiro ambaye pia Mbunge wa Uzini amesema kufanya hivyo kutasaidia kupunguza wimbi la vijana wanaojiingiza katika biashara za  dawa za kulevya na matumizi, ili tuweze kupata vijana wenye nguvu kwa maendeleo ya Taifa.

 

Naibu Waziri huyo ambae aliambatana na Viongozi wa Jimbo la Uzini, alitumia fursa hiyo kuwashauri  vijana kujikita katika Ujasiri amali ikiwemo shughuli za kilimo na ufugaji,na kuwacha kujiingiza katika mambo yasiofaa.

 

Wakati huo huo Mbunge na Mwakilishi walipata fursa ya kutembelea mradi wa kilimo cha umwagiliaji maji Mpunga na kilimo cha mboga mboga  katika Bonde la Chumbuni Shehia ya Uzini na kuzungumza na Wakulima wa Bonde hilo.

 

Mwakilishi wa Jimbo hilo Haji Shaaban Waziri, amewataka wakulima wa bonde hilo kuwa wastahmilivu wakati Viongozi wa Jimbo kwa kushirikiana na Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wanaendelea na jitihada ya kumalizia  ujenzi wa mitaro ya kusambaza maji katika Bonde hilo lenye wakulima zaidi ya miambili.

 

Amewaahidi wakulima hao kuwapatia fursa ya kuzungumza na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji,Maliasili na Mifugo, ili kuharakisha ujenzi wa  mitaro  na kuwapatia mafunzo ya kilimo cha Umwagiliaji  ili kuongeza kasi ya udhalishaji wa mazao.

 

Nao wananchi wakulima wa Bonde hilo wamewashukuru Viongozi hao kwa kuwatembelea na kujionea changamoto walizonazo sambamba na msaada wa mifuko ya saruji 20 waliopatiwa ili kumalizia ujenzi wa mitaro ya maji katika Bonde hilo.

 

Aidha wananchi wa Shehia ya Tunduni, wamewaomba viongozi wa Jimbo  kuzitafutia ufumbuzi wa haraka  changamo  ya  maji safi na salama, na umeme kwa baadhi ya mitaa ili waweze kufanya shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato na kupata maendeleo.

 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items