Mahakama moja ya Ecuador imemfutia uraia wa nchi hiyo mwasisi wa mtandao wa WikiLeaks Julian Assange. Gazeti la El Comercio limeripoti kwa kunukuu maelezo ya mahakama ya mjini Quito, kwamba yalifanyika makosa wakati mwasisi huyo wa Wiki Leaks mzaliwa wa Austarlia alipopewa uraia wa Ecuador mnamo mwaka 2017.
Assange bado anashikiliwa katika jela
yenye usalama mkubwa ya Belmarsh mjini London huko Uingereza. Marekani
inataka ikabidhiwe mfichua siri huyo. Assange amekuwa akikabiliwa na
tuhuma za kushirikiana na jaasusi wakijeshi wa zamani wa Marekani
Chelsea Manning kuvujisha mnamo mwaka 2010, taarifa za ndani za siri
kuhusu shughuli za vikosi washirika wa Marekani nchini Afghanistan.
Jumla ya mashtaka 18 yamefunguliwa na Marekani dhidi yake.Akikutwa na
hatia anaweza kukabiliwa na kifungo cha miaka 175 jela nchini Marekani.
Assange akimbilia katika ubalozi wa Ecuador mjini London mwaka 2012
kupuka kusafirishwa Marekani na alipewa hifadhi katika ubalozi huo na
baade kupewa uraia.
