NA THABIT MADAI,ZANZIBAR
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema Ofisi yake ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Meya wa jiji la Zanzibar ili kuirudishia hadhi yake Zanzibar.
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar,Mheshimiwa Othman Masoud Othman ameyasema hayo alipokutana na Meya wa jiji la Zanzibar, Mhe.Mahmoud Mohamed Mussa pamoja na ujumbe wake uliofika ofisini kwake Migombani Mjini Unguja.
Mhe Othman alisema "Watu kutoka maeneo mbali mbali yakiwemo Afrika ya Magharibi walikuwa wakija Zanzibar kwalengo la kujifunza namna ya kupanga mji (town and city plan) lakini kwa bahati mbaya sana kwasasa Zanzibar imepoteza sifa hio"
Aidha Mheshimiwa Othman amemuahidi Meya wa jiji la Zanzibar kwamba ofisi yake itatoa ushirikiano katika kuirudisha haiba ya Mji wa Zanzibar kwa kusema,
"Tupo tayari na tutaungana nanyi sio tu katika kuweka mazingira ya jiji la Zanzibar kuwa safi bali tutatoa msaada zaidi hata kuirudisha Zanzibar katika uzuri na haiba yake"
Meya huyo aliefika kwa Makamu wa Kwanza kwaajili ya kusalimia na kubadilishana mawazo, awali alikukutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Saada Salum Mkuya na Katibu mkuu wake Mhe. Khadija Khamis pamoja na Watendaji wa Ofisi hiyo.
Mhe. Othman amesema Ofisi yake itatoa ushirikiano wa dhati kwani taasisi hizi za Serikali zitafanikiwa zaidi zitakapokuwa na uzalendo wa kusaidiana katika kufikia malengo yake, kwani kuna muingiliano mkubwa wa majukumu hasa idara ambazo zipo chini ya ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais kama vile idara ya Mazingira, Idara ya watu wenye Ulemavu, Tume ya Ukimwi na Tume ya kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya.
Naye Meya wa jiji la Zanzibar, Mhe.Mahmoud, amemshukuru Makamu wa kwanza kwa nasaha zake pamoja na kuahidi kuitumia vyema fursa ya mashirikiano kutoka katika ofisi ya Makamu wa Kwanza ili kufikia malengo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Husein Ali Mwinyi, lakuufanya mji wa Zanzibar kuwa safi kwa kiwango kinachotakiwa.
Mhe. Sada Mkuya Salim, amemueleza Makamu wa kwanza kwamba awali kikaochao na Meya huyo wa Jiji kimeonesha mustakbali mwema kuelekea katika mashirikiano na idara zake jambo ambalo litaifanya Zanzibar kuwepo katika muenokano bora Zaid.
