NA THABIT MADAI, ZANZIBAR.
MUFTI Mkuu wa Zanzibar, sheikh, Saleh Omar Kaabi, amewataka viongozi wa dini, na masheha kuendelea kuhubiri amani kwa mujibu wa nafasi zao ili nchi iendelee kudumu kama ilivyokuwa sasa na ibaki kuwa salama.
Akizungumza katika mkutano wenye lengo la kudumisha amani ya nchi uliowashirikisha Maimamu, walimu wa madrasa na masheha wa Wilaya ya Magharibi ‘A, na ‘B’ iliyofanyika katika Ukumbi wa Msikiti wa Jamiu Zanzibar ulioko Mazizini nje kidogo na mji wa Zanzibar.
Alisema imani ya dini ya kiislamu inahitaji kuendelezwa, hivyo ipo haja kwa viongozi hao kuendelea kutoa taalamu katika misitiki, madrasa na shehia zao ili kudumisha madili na heshima ya Kizanzibar.
Alisema msingi wa dini ya kiislamu ni kuendeleza amani kwa mataifa mbalimbali hivyo ni vyema viongozi hao kuendelea kuhubiri amani na kuendelea kuwajaza waumini wao imani ya kweli.
Aidha alisema ni vyema viongozi hao kuendelea kushirikiana na viongozi wa nchi sambamba na kuwaombea dua katika sala zao hasa katika sala ya ijumaa jambo ambalo sio zambi kulifanya.
“Tukiendelea amani iliyokuwepo hata maendeleo yatakuwa yanakuja wenyewe bila ya kuzozana hili la kuwaombea dua viongozi wetu wa nchi ni jambo zuri kulifanya katika misikiti yetu kwani hupati vyambi” alisema.
Akizungumzia vitendo vya udhalilishaji ambapo kwa sasa vimeshika kasi katika nchi, ikiwemo kwa walimu wa madrasa, Mkufti Kaabi, alisema Ofisi yake, inatarajia kuandaa mpango maalum wa kuwafanyia uhakiki Maimamu na Walimu wa madrasa ili kujua tabia zao na kiwango chao cha elimu ili kuendana na elimu wanayoitoa kwa waamini.
Alisema hatua hiyo, itasaidia kuondosha walimu ambao hawana vigezo na hujiingiza katika vitendo vya udhalilishaji kwa wanafunzi.
Nae Katibu wa Mufti Zanzibar, shekh Khalid Ali Mfaume, alisema kuendeleza kwa vitendo vya udhalilishaji ndani ya taasisi za dini ni kuitia doa dini na viongozi hao kutoaminiwa na wananchi.
Hivyo, alisema, Waendeleze Umoja haipendezi Kuna viongozi wa dini kuweka mijadiliano yasiyokuwa na maana ambavyo vinasababisha kuwepo mifarakano kwa waumini Wao.
Alisema Ofisi ya mufti hairidhiki kuona baadhi ya Misikiti na ajenda ya kutomuombea dua Rais wa Zanzibar na wengi wao wamekuwa wakihibiri misimamo na sio dini jambo ambalo halifai katika uislam na badala yake wamekuwa na misimamo ya kuwalaani viongozi wao wa nchi jambo ambalo halipendezi.
“Jambo hilo halipendezi na Ofisi ya Mufti halitufurahishi na tunalilaani kwa kweli hili lipo, hivyo ni vyema likaachwa ara moja” alisema.
Sambamba na hilo, Sheikh Khalid, alisema kuwa pia kumekuwepo kwa tabia ya baadhi ya viongozi wa dini ya kiislamu wamekuwa wakilumbana katika mitandao ya kijamii jambo ambalo halifai na halikubaliki kubwa linawapotezea heshima zao za kiuongozi.
Kwa upande wa Mashehe, Katibu Khalid, aliwataka kutokubali kuruhusu ujenzi wa misikiti katika Shehia za hadi wapate kibao kutoka ofisi ya Mufti ili kuweza kuepusha misikiti kujaa katika shehia moja huku shehia nyengine zikiwa zinahitaji.
Mkuu wa fatwa katika ofisi ya mufti Zanzibar, shekh thabit noman jongo, alisema, ni vyema jamii kushirikiana katika kuondosha maovu yanayojitokeza nchini ili kudumu kwa amani ya nchi.
Nae, Katibu wa Rafiki wa Zanzibar, Abubakari Kabogi, aliwahimiza Waislamu kuendelea kuwatii viongozi ili kuimarisha upendo, mshikamano, utulivu na maridhiano.
Nao washiriki wa mkutano huo wamewataka maimamu kubadilika katika kutoa hutuba zitakazoendana na matukio yanayotokea katika jamii na kuweza kuondoka.
Pamoja na hayo, wamekiri kuwepo kwa tabia ya baadhi ya misikiti kutomuombea dua Rais wa Zanzibar jambo ambalo halipendezi katika jamii kwani Rais amekuwa akifanya jitihada mbalimbali ili amani iweze kupatikana nchini.
Hivyo, alisema wakati umefika kwa ofisi ya Mufti kuandaa miongozo ya hotuba za ijumaa katika misikiti mbalimbali ili mitafaruku yaweze kuondoka ambapo hotuba za sasa zimejaa mbwembwe na nyengine kuwapotosha waumini wao.
