Bei ya pamba yavunja rekodi ya miaka 20


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, amesema kuwa wakati msimu wa ununuzi wa pamba mwaka huu ukielekea ukingoni, bei ya zao hilo imepanda kutoka Sh 1,050 kwa kilo ambayo ilitangazwa na Serikali kupitia bodi ya pamba hadi Sh 1,800.

Mei 10, 2021 Bodi ya Pamba ilitangaza bei elekezi ya ununuzi wa zao hilo kuwa ni Sh 1,050, ambapo mkuu huyo amesema kupanda kwa kiwango kikubwa cha bei hiyo sababu kubwa siyo bei kupanda katika soko la dunia pekee.

Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Kisesa katika kijiji cha Mwaukoli, Kafulila amesema kuwa kwa mwaka huu bei imepanda kwa kiwango kikubwa kuliko misimu mingine yote takribani miaka 20 iliyopita.

Amesema kwa mara ya kwanza wakulima wa zao la pamba mkoa wa Simiyu wameuza pamba yao kwa Sh 1,800, huku akieleza kuwa sababu kubwa imetokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kudhibiti mbinu chafu zilizokuwa zikifanywa na wanunuzi wa pamba.

“Bei nzuri ya pamba nchini mwaka huu ni matokeo ya uongozi thabiti wa awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu, wanaodhani sababu ni ongezeko la bei kwenye soko la dunia pekee hawako sahihi.

“Watu wanapaswa kufahamu kuwa bei ya soko la dunia kwa sasa ni dola senti 90, hata mwaka 2013, 2018 bei ilikuwa hiyo hiyo kwenye soko la dunia, lakini kwa bei ya ndani haijawahi kufikia kiwango cha sh. 1,800 kwa kilo,” amesema Kafulila.

Amesema Rais Samia ameweza kudhibiti mbinu chafu za wanunuzi wa pamba ikiwemo kukomesha umachinga katika zao hilo, hali ambayo imechangia bei ya mwaka huu kuvunja rekodi ya bei kwa karibu miaka 20.

Baadhi ya wananchi katika kijiji hicho, wamekiri kuuza amba yao kwa Sh 1,800 kwa kilo huku wakibainisha kuwa haijawahi kutokea bei ya pamba kupamba kwa kiwango hicho.

Wananchi hao wameipongeza serikali kwa kusimamia suala la bei ya pamba, hali ambayo imesababisha wengi wao kuhamasika kulima zaidi zao hilo katika msimu mpya wa zao hilo mwaka huu.


Post a Comment

0 Comments