Spika Ndugai atoa kauli kwa vijana, kamati za Bunge



Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ametoa wito kwa Asasi za Kiraia zinazojishughulisha na kuwawezesha vijana kiuchumi nchini kufanya kazi na Kamati za Bunge mbalimbali kwa lengo la kuwasilisha maoni ya vijana katika kuanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayosaidia kuwawezesha vijana kiuchumi.


Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa, alitoa wito huo jana Jumamosi Oktoba 23, 2021, alipotembelea Banda la Asasi ya Vijana - Africa Youth Transformation Tanzania, wakati wa Maonyesho ya Wiki ya Azaki yanayofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Tanzania.


Spika huyo amesema; “Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya kuwajengea uwezo vijana kwa kuwapatia elimu mbalimbali kuhusu namna ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi na hatimaye kutoa mchango wa maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Ndugai ambaye ndie alikuwa Mgeni Rasmi wa Maonyesho hayo kwa mwaka huu.


Hivyo basi, Ndugai amezishauri Asasi za Vijana nchini kudumisha mahusiano mazuri na Kamati za Bunge hususani zinazosimamia masuala ya vijana na uchumi ili wapate fursa ya kuwasilisha maoni mbalimbali yanayotolewa na vijana kuhusiana na namna gani Serikali kupitia Wizara husika inaweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana ikiwamo ukosefu wa ajira za kudumu.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana – AYT, Justine Mponda amemueleza Ndugai kwamba Taasisi yake kwa kushirikiana na taasisi ya Open Mind Tanzania, imekuwa ikifanya kazi za maendeleo na Halmashauri mbalimbali nchini kwa muda mrefu zikiwamo za kutoa mafunzo ya ujasiriamali na matumizi bora ya fedha katika biashara.


“Tunawahamasisha vijana jinsi gani wanaweza kupata fedha za maendeleo kupitia mikopo inayotolewa na Halmashauri na taasisi za kifedha nchini. Pia kupitia mafunzo haya, tunazalisha wataalamu vijana katika Sekta za Biashara, Afya, Kilimo na nyingine za maendeleo,” amesema Mponda wakati alipokuwa anatoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na taasisi yake katika kuwawezesha vijana nchini kiuchumi.


Pia Meneja wa miradi wa AYT, Arafat Lesheve ameahidi kuendelea kuwafikia vijana katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha kwa kuwapatia ujuzi, kuhamasisha ushiriki wao katika kuleta maendeleo endelevu yenye tija na utumiaji mzuri wa teknolojia na mitandao ya kijamii.


“Tunatoa pia elimu ya namna gani ya kutumia vizuri hela zinazotolewa na taasisi za kifedha na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Vijana, Kazi na Watu wenye Ulemavu kupitia Halmashauri kwa lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi,” ameongeza Lesheve.


Takwimu zinaonyesha asilimia 60 ya idadi yote ya watu nchini Tanzania ni vijana ambao ni tegemeo la Taifa kwa siku za usoni.

Maonyesho ya Azaki mwaka huu yalitanguliwa na maandamano yaliyoandaliwa na Shirika la Asasi za Kiraia nchini Tanzania (FCS), yaliyojumuisha maelfu ya wawakilishi kutoka Asasi za Kiraia mbalimbali zinazofanya shughuli za kimkakati kwenye Sekta mbalimbali nchini na wadau wengine wa maendeleo.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi