https://monetag.com/?ref_id=TTIb Bomoabomoa Mbweni yapigwa 'stop' | Muungwana BLOG

Bomoabomoa Mbweni yapigwa 'stop'

 


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesitisha bomoabomoa iliyokuwa inaendelea maeneo ya mpakani mwa Bunju na Mbweni.


Amechukua uamuzi huo jana Novemba 24,2021 alipotembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi.


Siku mbili zilizopita wakazi wa eneo hilo walieleza kupambana na  polisi na maofisa ardhi  waliofika kubomoa nyumba zao na kueleza kuwa hayakuwa maagizo ya mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe waliyokubaliana naye katika kikao chao cha kulijadili suala hilo.


Akitoa uamuzi baada ya kusikiliza malalamiko,  Makalla amesema ubomoaji huo usitishwe kwanza na hakuna atakayeruhusiwa kujenga chochote kwa sasa hadi hapo timu yake itakapofika na kusikiliza mapendekezo ya wananchi yatakayowasaidia  kutoa uamuzi kwa maslahi ya pande zote.


Pia, alinuaguza mkuu wa kituo cha polisi Mbweni kuhakikisha  polisi  wote walioshikiliwa katika kituo cha polisi kutokana na kuibuka kwa mgogoro huo kuachiwa.


Mmoja wa wakazi hao,  Mwajuma Mfaume amesema kwa kuwa baadhi walishaendeleza kwa kujenga nyumba za kudumu, wanaiomba Serikali iwafikirie kuwapa maeneo kabla ya kuwahamisha, lakini wakashangaa ubomoaji wa kutumia mabavu ukifanyika.


Mkazi mwingine,  Eva Mathias amesema hivi sasa  upimaji unaofanywa wa viwanja katika eneo hilo ni mita za mraba 50 kwa 50 na malipo yake ni fedha nyingi ambazo wao  hawawezi kumudu lakini kwa kuwa walishajenga, alishauri Serikali iangaliwe namna wapimiwe vipimo watakavyovimudu wananchi wa hali ya chini.


Salum Hashim, amesema walipewa eneo hilo mwaka 2005 kwa ajili ya shughuli za kilimo na wafugaji lakini baadaye Serikali ikalitwaa na kukata viwanja na hata mgogoro wa juzi ulivyoibuka waliahidiwa kuwa waandike namba kwa ajili ya kutafutiwa maeneo mengine.


“Lakini ndio tunashangaa kilichofanyika ni kuja  kubomolewa nyumba na  kupigwa mabomu yaliyosababisha wengine kulala nje na watoto hadi leo na wengine wakiwa wanashikiliwa na jeshi la Polisi,” amesema Hashim.


Awali Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Idrisa Kayera amesema eneo hilo Serikali ilichukua kwa wananchi na kuwalipa fidia licha ya kuwa zilichelewa kutolewa jambo lililochangua watu wengine kuvamia baadaye.


Amesema hivi sasa wameamua kuliendeleza eneo hilo kwa kurudisha alama ambazo wananchi walizing'oa ili kuanza kuuza viwanja hivyo ambapo fedha  zake walizikopa na wanatakiwa kuzirejesha.


Akizungumza namna walivyopokea maamuzi ya Makalla, fredrick Edward ambaye ni kiongozi wa wananchi hao amesema ni jambo zuri kwani kuna wananchi 186 mpaka sasa wameathirika na bomoabomoa hiyo huku nyumba 59 zikiwa zimebomolea.

Post a Comment

0 Comments