F Rugemalira ajiweka njiapanda | Muungwana BLOG

Rugemalira ajiweka njiapanda


Mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemalira anayetaka kuzishtaki taasisi za kifedha, kampuni na watu binafsi anaowatuhumu kuiibia na kuisababishia Serikali hasara ya matrilioni ya pesa, sasa yuko njiapanda ikiwa Serikali haitaingilia kati kumsaidia.


Hali hiyo inatokana na taratibu za kuwashtaki watuhumiwa walioko nje ya nchi, ikiwamo kuwapelekea wito wa kufika mahakamani, jambo ambalo linaweza kuwa kikwazo kutimiza azma hiyo kwa kuwa sheria inamnyima mamlaka yeye binafsi kukamilisha mchakato huo isipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pekee.


Rugemalira amefungua maombi ya kibali cha kufungua na kuendesha mashtaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, mkoa wa Dar es Salaam.


Katika mchakato huo Rugemalira ambaye ni mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, amefungua maombi hayo dhidi ya wadaiwa 11.


Maombi hayo yalitajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo jana, lakini wajibu maombi hawakuwapo kutokana na kutopewa nyaraka na taarifa za shauri hilo pamoja na hati ya wito wa kufika mahakamani.


Wakili Gaspar Nyika kutoka kampuni ya uwakili ya Immma Advocates, aliyefika mahakamani hapo kwa niaba ya wajibu maombi, aliieleza mahakama kuwa waombaji walikosea kuwapelekea nyaraka za kesi na wito wa kufika mahakamani.


Nyika aliikumbusha Mahakama kuwa waombaji hao wanapaswa kuwapelekea hati hizo wajibu maombi huko walipo.

Post a Comment

0 Comments