F Kijana Ajinyonga Baada ya Kuelezwa Hawafai Kuoana kwa Sababu ya Undugu | Muungwana BLOG

Kijana Ajinyonga Baada ya Kuelezwa Hawafai Kuoana kwa Sababu ya Undugu


Na John Walter-Babati

Karimu Said (31), mkazi wa Singida, amefariki dunia kwa kujinyonga katika kijiji cha Matufa, kata ya Magugu wilayani Babati mkoani Manyara, baada ya kudaiwa kuvunjika moyo kutokana na taarifa kuwa mwanamke aliyekuwa naye kwenye mahusiano ni ndugu yake wa upande wa shangazi, hivyo hawakufaa kuoana.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea alfajiri ya leo katika kitongoji cha Kichangani, ambapo marehemu alikutwa akining’inia juu ya mti nyuma ya nyumba ya mpenzi wake, Mwanaidi Hamis Jumanne, ambaye anaishi hapo na watoto wake.

Kwa mujibu wa Mwanaidi, waliokuwa kwenye mahusiano kwa takribani mwezi mmoja, marehemu Karimu alifika nyumbani kwake usiku na kuaga kuwa anaelekea kazini kwake katika kiwanda cha Manyara Sugar. Hata hivyo, kabla ya tukio hilo, alisema kuwa alionesha mabadiliko ya tabia na mawazo mengi mara baada ya kuambiwa kuwa wao ni ndugu na hawafai kuoana.

“Aliniambia, ‘kama sitakuwa na wewe ni heri nife mimi au wewe’, lakini sikudhani kama anaweza kufanya hivyo,” alisema Mwanaidi kwa huzuni.

Kwa mujibu wa taarifa, wawili hao walifahamiana mwezi mmoja uliopita kabla ya kugundua kuwa wana undugu wa karibu upande wa shangazi, jambo ambalo liliwaumiza na kuathiri mwenendo wa mahusiano yao.

Mwenyekiti wa kijiji cha Matufa, Shabani Kondo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa familia ya Karimu ambaye ni mkazi wa Singida imeshafahamishwa, huku Jeshi la Polisi likifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu kwenda kuhifadhiwa katika kituo cha afya Magugu kwa taratibu zaidi.

Majirani na wakazi wa eneo hilo wameeleza masikitiko yao juu ya tukio hilo, wakiwataka vijana kuwa wavumilivu na kutafuta msaada wa kisaikolojia badala ya kuchukua maamuzi magumu wakati wa mitihani ya kihisia na maisha.


Post a Comment

0 Comments