Taliban yazuia vipindi na filamu za mapenzi kwenye runinga

 


Serikali ya Taliban nchini Afghanistan imetoa mwongozo mpya wa kidini unaozitaka runinga za nchini Afghanistan kuacha kuonyesha vipindi na tamthilia za mapenzi zinazowashirikisha waigizaji wanawake.


Katika agizo la kwanza kwa vyombo vya habari vya Afghanistan lililotolewa na wizara ya kukuza uadilifu na nidhamu, Taliban pia imewataka waandishi habari wa kike kuvaa vazi la hijabu wakati wanapotangaza. Wizara hiyo pia imezitaka runinga za nchini humo kutopeperusha vipindi vinavyomuonyesha Mtume Mohammed, na viongozi wengine wanaoheshimika. 


Pia imetaka kupigwa marufuku filamu na vipindi vinavyokwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu na tamaduni za Afghanistan. Msemaji wa wizara hiyo ya kukuza uadilifu Hakif Mohajir ameliambia shirika la habari la AFP kuwa hizo sio sheria bali ni mwongozo wa kidini. Mwongozo huo mpya ulisambazwa jana Jumapili kwenye mitandao ya kijamii.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi