Dkt. Mpango awaasa wahitimu kutumia vyema Taaluma zao



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka wahitimu wa Vyuo Vikuu  kutumia vema elimu wanayopata  kuleta tija kwa Taifa na jamii kwa ujumla katika kukuza uchumi wa nchi.
 
Dkt. Mpango ameyabainisha hayo  Jijini Mwanza  wakati wa mahafali ya 41 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ambapo amesema lazima wahitimu hao kutumia taaluma yao katika kujiletea maendeleo.

Aidha, Mhe. Mpango ameagiza Wizara ya Elimu kuhakikisha  vituo vyote vya Chuo hicho vinaunganishwa na mkongo wa Taifa ili kuwezesha matumizi ya TEHAMA na kupunguza gharama za uendeshaji .

"Vituo vyote vya Chuo Kikuu Huria  vitaunganishwa na mkongo wa Taifa na  hili naagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha linafanyika mara moja ili kupunguza gharama za uendeshaji," ameongeza Mhe. Mpango

Awali akiongea katika mahafali hayo, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema Chuo Kikuu Huria  kimetengewa fedha kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya  ujenzi wa miundo mbinu, kusomesha wahadhiri na miradi mingine.

"Serikali kwa kutambua mchango wa Chuo  Kikuu Huria katika kupeleka elimu kwa jamii kupitia mradi wa HEET tutajenga maabara saba katika mikoa ya Njombe, Arusha, Dodoma, Mwanza, Kigoma, Mtwara na Pwani ambazo zitajikita katika tafiti za kisayansi kulingana na shughuli na mahitaji muhimu ya eneo husika," amefafanua Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kujenga vituo vya Chuo Kikuu Huria katika mikoa ya Geita, Kigoma, Lindi, Simiyu na Manyara ambao mikoa hii ilikuwa ikitumia majengo ya kukodi kwa gharama kubwa.

Zaidi ya Wahitimu 4,000 wametunukiwa Shahada mbalimbali zikiwemo Shahada Umahiri na Uzamivu wakiwemo wanafunzi kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ghana, Malawi, Zambia, Congo, Namibia na Ethiopia. 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi