Na Ahmad Mmow, Lindi.
Wananchi nchini wameombwa kuendelea kuchangia mfuko wa udhamini wa kudhibiti UKIMWI (ATF) ili kupunguza utegemezi.
Wito huo umetolewa leo katika manispaa ya Lindi na naibu waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu kazi, ajira, vijana na wenye ulemavu, Patrobas Katambi ambae alikuwa mgeni rasmi wa mbio za ATF marathon 2022.
Waziri Katambi alisema kampuni, asasi mbalimbali na wananchi hawanabudi kuendelea kuchangia mfuko huo. Kwani ustawi wake utapunguza utegemezi na uendelevu wa uwezo wa mapambano dhidi ya UKIMWI.
Alisema kumekuwa na mafanikio kupitia mfuko huo. Kwani fedha zilizokusanywa na kuwekwa ni takribani shilingi bilioni 4.9 ambazo zimepelekwa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya shughuli za udhibiti, upatikanaji wa dawa za kufubaza Virusi Vya UKIMWI na kutekeleza afua za kinga dhidi ya maambukizi mapya.
Alitaja baadhi ya matumizi mengine yaliyofanyika kupitia fedha hizo kuwa ni shilingi milioni 535 zilizopelekwa kwa vyuo vya elimu ya juu kwa dhamira hiyo ya kudhibiti maambukizi mapya ya VVU kwa vijana.
Alibainisha kwamba mkakati mkubwa wa taifa nikuwakinga vijana na maambukizi mapya ya UKIMWI. Huku akieleza sababu ya kuelekeza nguvu kubwa kwa kundi la vijana.
Miongoni mwa sababu alizotaja ni pamoja na vijana kuwepo katika sekta nyingi za uzalishaji mali na uchumi nakufanya kundi hilo la vijana ni nguvu kazi muhimu kwa taifa.
Aidha aliweka wazi kwamba serikali inafanya juhudi kubwa ya kuimarisha mfuko huo. Nibaada ya kubaini kwamba ufadhili umepungua na mwelekeo wa fedha kutoridhisha kutokanana sababu mbalimbali. Ikiwemo ugonjwa wa ebola, vita baina ya baadhi ya mataifa duniani na mtikisiko wa uchumi.
Hatahivyo waziri Katambi alihadharisha na kutoa wito kwamba ili juhudi hizo ziweze kufanikiwa nilazima makundi yote yafikiwe na juhudi hizo ziwe za pamoja. Kwani vijana wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi mapya.
Kuhusu wanaoishi na VVU alitoa wito kwa watu hao wafuate, wazingatie na kutekeleza kwa vitendo maelekezo na ushauri wanaopewa na wataalamu wa afya.
