Raia wa Ukraine wanaendelea kuyahama makaazi yao kutokana na mashambulizi ya Urusi. Haya ni kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Afisa mmoja wa shirika hilo, Violaine des Rosier, amewaambia waandishi wa habari kuwa wanatarajia idadi ya wanaoondoka kuongezeka katika miezi michache ijayo kwani mji wa Kyiv tayari unaanza kuwa mtupu.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wahamiaji linasema nusu ya mji wa Kyiv hauna nguvu za umeme na kwamba watu wanaoishi katika nyumba zenye ghorofa za juu hawawezi kupata huduma za maji kwa kuwa shinikizo la kuyafikisha maji katika ghorofa hizo liko chini mno.
Lakini Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR linasema halijaona ongezeko la wakimbizi wanaovuka mpaka wa Ukraine.
