Upinzani wa mrengo wa kulia nchini Uhispania umeghadhabishwa na hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kutaka kuondoa uchochezi kama mashtaka. Chama cha Popular Party na kile cha Vox Party vinasema hatua hiyo itakuwa ni kama zawadi kwa vyama vinavyotaka kujitenga, na ni kwa ajili ya serikali kupata uungwaji mkono bungeni.
Hapo jana bunge nchini humo liliidhinisha mswada wa kufanyia mabadiliko sheria ya uhalifu kwa ajili ya kuondoa kile kinachoonekana na serikali ya mrengo wa kushoto ya Uhispania, kama sheria ya zamani na kuibadilisha na sheria inayoambatana na maadili ya kisasa ya Ulaya.
Kulingana na vyombo vya habari nchini Uhispania, mabadiliko hayo yanatarajiwa kabla ya mwisho wa mwaka huu. Mashtaka ya uchochezi ndiyo yaliyokuwa yamefunguliwa kiongozi wa zamani wa Catalunya, Carles Puigdemont, na wenzake na kuwapelekea kuihama nchi hiyo wakihofia kifungo jela.
Jimbo la Catalunya lilikuwa linataka kujitenga na Uhispania na kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa nchini humo kwa miongo kadhaa.
