Kampuni ya teknolojia ya Marekani ni 'hatari kwa usalama wa taifa' - China

 


China inasema bidhaa zinazotengenezwa na kampuni ya teknolojia ya Marekani, Micron Technology ni hatari kwa usalama wa taifa.


Mamlaka ya udhibiti wa anga ya mtandao nchini humo ilitangaza siku ya Jumapili kwamba kampuni hiyo ambayo ni mtengenezaji mkuu wa chipu nchini Marekani ni "hatari kubwa kwa usalama wa mtandao".


Inamaanisha kuwa chipu za kampuni hiyo zitapigwa marufuku kushiriki katika miradi muhimu ya miundombinu katika nchi hiyo ambayo uchumi wake ni wa pili kwa ukubwa duniani.


Hii ni hatua ya kwanza kuu ya China dhidi ya kampuni hiyo kubwa ya teknolojia ya Marekani, huku mvutano ukiongezeka kati ya Beijing na Washington.


"Uchunguzi umegundua kuwa bidhaa za Micron ni tishio kwa usalama wa mtandao, zinahatarisha usalama wa mfumo muhimu wa usambazaji wa miundombinu ya habari ya Uchina, na zinaweza kuathiri usalama wa kitaifa wa China," Mamlaka ya usimamizi wa Mtandao wa China (CAC) ilisema katika taarifa.


Ikijibu madai hayo, serikali ya Marekani ilisema itafanya kazi na washirika kushughulikia kile ilichokiita "upotoshaji wa soko la chipu kumbu kumbu uliyosababishwa na vitendo vya China".


"Tunapinga vikali vikwazo ambavyo havina msingi," msemaji wa Idara ya Biashara ya Marekani alisema.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi