Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesisitiza kuwa mji wa Bakhmut "haujatekwa" na Urusi baada ya kundi la mamluki linaloungwa mkono na Moscow kudai udhibiti.
Zelensky alisema hayo katika hotuba yake katika mkutano wa kilele wa G7 huko Hiroshima, Japan.
Mwanzilishi wa Wagner Yevgeny Prigozhin hapo awali alidai ushindi huko Bakhmut.
Lakini vyanzo vya kijeshi vya Ukraine viliiambia BBC kuwa bado wana udhibiti wa majengo machache nje kidogo ya mji.
Katika mkutano na waandishi wa habari katika siku ya mwisho ya mkutano huo, Bw Zelensky alikataa kutoa maelezo sahihi. Lakini alisema mji huo, ambao umekumbwa na vita vya muda mrefu vya umwagaji damu tangu Agosti, "haujatekwa" na Urusi "hadi leo".
"Hakuna tafsiri mbili au tatu za maneno hayo," aliongeza, baada ya mkanganyiko wa awali kuhusu matamshi yake juu ya hatima ya jiji hilo.
Siku ya Jumamosi video iliyosambazwa mtandaoni ilimuonyesha mkuu wa Wagner Bw Prigozhin wa akidai kuwa wapiganaji wake - ambao wameongoza shambulio la Urusi dhidi ya Bakhmut - walikuwa wakidhibiti kikamilifu jiji hilo.
Bw Zelensky alilinganisha mji wa Bakhmut na Hiroshima, ambayo ilishambuliwa na bomu la atomiki katika Vita vya Pili vya Dunia, na kuahidi "ujenzi" kama huo wa nchi yake.
Vita nchini Ukraine vimetawala mkutano wa siku tatu wa viongozi wa G7 nchini Japan, huku Bw Zelensky akikutana na viongozi kadhaa wa dunia kuomba uungwaji mkono zaidi.
