Bilioni 4.1 kujenga shule ya wvulana Manyara.Na John Walter -Babati

Wakati Ujenzi wa shule ya wasichana Manyara ikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi huku Wanafunzi wakitarajiwa kuingia Julai mosi mwaka huu, Serikali imetoa Bilioni 4.1 kujenga shule ya wavulana.

Shule hiyo ya Sekondari ya wasichana Manyara (Manyara girls) iliyogharimu shilingi bilioni 3 ni ya Bweni kwa  Masomo ya Sayansi kupitia Mradi wa kuboresha elimu ya Sekondari (SEQUIP).

Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amesema wamepata neema nyingine tena kutoka kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya Shilingi Bilioni 4.1 kujenga shule ya Bweni ya wavulana katika wilaya hiyo.

"Hakika Manyara tuna bahati lakini kipekee wilaya ya Babati na mimi kama mkuu wa wilaya kwa kweli najisikia fahari sana kuwa sehemu ya mapinduzi ya elimu chini ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita" alisema Twange

Twange ametoa ahadi kwa Rais Samia Suluhu Hassan na mkuu wa mkoa wa Manyara, kusimamia vyema fedha hizo zitumike kama ilivyokusudiwa.

 "Kama nilivyosimamia shilingi bilioni 3, nitafanya hivyo pia katika shilingi Bilioni 4.1 zilizoingia kwa umakini mkubwa kwa kushirikiana na halmashauri" alisema Twange

Mkoa wa Manyara una wilaya tano na halmashauri saba, halmashauri ya mji wa Babati imepata shule ya wasichana na halmashauri ya wilaya inajenga shule ya wavulana.


 

Post a Comment

0 Comments