Watu wanne wakamatwa wakitorosha mifugo 70 kwa njia panya


Na. Abel Paul, Jeshi la Polisi – Namanga- Arusha

Jeshi la Polisi kikosi cha kuzuia wizi wa Mifugo kwa kushirikiana na wizara ya mifugo na uvuvi wamefanikiwa kukamata watuhumiwa wanne na mifugo 70 aina ya Ng’ombe ambayo ilikuwa ikitoroshwa Kwenda nchi Jirani kinyume na utaratibu huku likitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na tabia hiyo.

Akitoa taarifa hiyo leo Juni 10,2024 wilayani Longido Mkoa wa Arusha Kamanda wa Polisi Kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua amesema kikosi hicho kinaendelea na Operesheni yake nchi nzima ya kuwabaini baadhi ya watu wanaotorosha mifugo na kukwepa taratibu zilizopo.

SACP Pasua amesema watuhumiwa hao waliokamatwa wakisafirisha mifugo hiyo sabini majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi huku akiweka wazi kuwa kikosi hicho tayari kina majiana ya watu wanajihusisha na utoroshaji wa mifugo ambapo amesema watuhumiwa hao pia watakamatwa wakati wowote.

Kamanda Pasua amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu wanaojihusisha na utoroshaji wa mifugo ili Jeshi hilo liwachukulie hatua za kisheria wahusika wa vitendo hivyo.

Nao baadhi wananchi wamesema kuwa watu ambao watabainika kuhusika katika matukio hayo wanapaswa kukamatwa na vyombo vyao vya usafiri wanavyotumia kutaifishwa ili matukio kama hayo yaweze kupungua hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments