Karim Foundation waahidi kutoa Fedha zaidi miradi ya Maendeleo Arri na Ayalagaya.


Na John Walter -Babati 

Mahusiano mazuri yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yameendelea kuonekana kwa vitendo.

Hayo yamesemwa Julai 6, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Mhe. Daniel Sillo wakati akizungumza na Wananchi wa Kata za Arri na Ayalagaya kwenye hafla ya kuwaaga wadau wa Maendeleo Taasisi ya Karim Foundation waliofika nchini hapa kwa mapumziko ya wiki mbili.


Mhe. Sillo amesema nchi itaendelea kudumisha amani na utulivu uliopo ili wawekezaji na wafadhili mbalimbali wafanye kazi zao bila hofu, hivyo amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua nchi, kuwavutia wawekezaji, kudumisha ulinzi na usalama na kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta zote."Nchi kama haipo salama huwezi kupata wafadhili kama hawa na kuwekeza pesa nyingi kiasi hiki" Alisema Mhe. Sillo

Aidha Mhe. Sillo amewaomba wakazi wa maeneo hayo ambayo yupo Mfadhili huyo waendelee kuboresha mahusiano mazuri yaliyopo ili aendelee kuwepo pia kuendelea kutunza miradi yote ambayo imeletwa katika maeneo yao.

Naye Mkurugenzi wa Kimataifa wa Taasisi ya Karim Foundation Nelson Mattos, amesema ataendelea kutoa fedha kutoka kwa Wadau wake lengo likiwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Babati Vijijini Ndg. Jackson Hhaibey amewapongeza wadau hao kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo iliyonadiwa kwenye Ilani ya Chama chake.

Post a Comment

0 Comments