F Maelfu wafikiwa na Madaktari bingwa wa Dkt Samia. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Maelfu wafikiwa na Madaktari bingwa wa Dkt Samia.



Na John Walter -Babati 

Takribani Wagonjwa 3,278 mkoani Manyara wamefikiwa na kupatiwa huduma za matibabu na timu ya madaktari bingwa wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wanaowafuata wananchi katika maeneo yao kuwapunguzia gharama za kusafiri kwenda mbali kufuata huduma za kibingwa.

Akifunga kambi hiyo septemba 28,2024  katika kituo cha afya Magugu wilayani Babati, mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema  Serikali imeendelea kuboresha miundombinu kwenye zahanati, vituo vya afya, hospitali na nyumba za waganga ili huduma itolewe kama inavyostahili.

Sendiga amesema huduma hizo zimewasaidia Wananchi kupata huduma za afya kwa Karibu na kuwapunguzia gharama ambazo wangezitumia kwenye usafiri na kulala wakati wakifuata huduma hizo hospitali mbalimbali nchini.

"Namshukuru Sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa aliyonayo katika maboresho kwenye sekta ya afya" alisema Sendiga 

Naye Naibu katibu mkuu wizara ya afya Dr.Ismail Rumatila amesema Mei 6,2024, wizara ya afya kwa kushirikiana na ofisi ya Rais ,tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) ilizindua Mpango huo kabambe wa madaktari bingwa wa Rais Dkt Samia ambao unatekelezwa kwa ushirikiano na mkoa na Halmashauri za wilaya zote nchini.

Dkt Rumatila amesema madaktari bingwa hao tayari wamewafikia wateja 69,797 nchi nzima.

Malengo ni kusogeza huduma za kibingwa na kibobezi katika ngazi ya afya ya msingi kwenye hospitali zote za ngazi ya halmashauri, kuwajengea uwezo watumishi katika kutoa huduma bora za afya ya uzazi, mama na mtoto, upasuaji na magonjwa ya ndani.

Huduma hizo zinaongozwa na Kauli mbiu isemayo " Madaktari bingwa wa Dkt Samia tumekufikia, karibu tukuhudumie" 

Madaktari bingwa hao wa Mama Samia  walipiga kambi wilaya ya Babati kwa siku sita na kutoa huduma za afya za kibobezi kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo ya njia ya uzazi na watoto.

Aidha wametoa huduma kwa wagonjwa ya wanawake ,dawa za usingizi ,upasuaji wa kibobezi na magonjwa ya kawaida.

Post a Comment

0 Comments