F Uchaguzi wa Serikali za mitaa umeiva Babati vijijini. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Uchaguzi wa Serikali za mitaa umeiva Babati vijijini.



Na John Walter -Babati 

Jumla ya vijiji 102, vitongoji 408 vya Halmashauri ya wilaya ya Babati vitachagua viongozi wapya katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Mwezi Novemba 27,2024.

Viongozi watakaochaguliwa kwa kupigiwa kura na wananchi ni wenyeviti wa vijiji, vitongoji na wajumbe 25 wa Halmashauri ya Kijiji kwenye kila Kijiji ambapo kati yao theluthi Moja wanatakiwa kuwa Wanawake kwa mujibu wa Sheria.

Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya  Babati Anna Mbogo amesema zoezi la uandikishaji litaanza Oktoba 11 hadi Oktoba 20 na kampeni kwa wagombea zitaanza Novemba 20  saa mbili asubuhi hadi Novemba 26 saa kumi na mbili jioni.

Aidha wenye umri wa kuanzia miaka 21 wanahimizwa kwenda kuchukua fomu za kugombea nafasi za uwenyekiti kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa, Oktoba 25 itakuwa ni ukomo wa Viongozi wa kijiji na vitongoji waliopo madarakani kwa sasa.

Akitoa maelekezo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa septemba 26,2024, Mbogo amewataka  viongozi wa vyama vya  siasa  kufanya kampeni safi za kistaarabu zenye kujenga hoja na kudumisha amani ya nchi wakati wote  wa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa tarehe 27/11/2024.  



Kwa Upande wake katibu Tawala Wilaya ya Babati  Halfan Matipula amewasisitiza  viongozi wa vyama vya siasa kuheshimiana na kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa kuzingatia sheria taratibu na kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa  2024.

Nao Viongozi wa kisiasa Daniel Tango mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na Luka Felisian Doga Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF wilaya ya Babati vijijini pamoja na katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Babati Filbert Mdaki wameiomba serikali isimamie kikamilifu uchaguzi huo ili uwe huru na salama.

TAKUKURU wilaya ya Babati imewataka wasimamizi wawe makini kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi huo.

Kwenye kikao hicho cha Maelekezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa  vyama vya siasa, Viongozi wa Taasisi na wasimamizi ngazi za Kata na vijiji katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Babati uliopo kata ya Arri.

Post a Comment

0 Comments