Sillo : Serikali kuendelea kuwahudumia Wananchi kwenye nyanja zote.



Na John Walter -Babati 

Mbunge wa Jimbo la Babati vijijini  Mhe.Daniel B. Sillo  amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imejipanga vyema kuendelea kutoa huduma kwa wananchi katika nyanja zote.

Mhe. Sillo ametoa kauli hiyo kwenye Mkutano wa hadhara wakati akisikiliza na kutatua kero za Wananchi katika Kijiji cha Saydoda kata ya Ufana  ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake Jimboni humo.

Wananchi hao ambao wengi ni Wakulima amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kutoa pembejeo za kilimo na mbolea kwa bei nafuu ya ruzuku.


Katika Suala la Umeme Mhe.Sillo amesema tayari miundombinu ya Umeme imewekwa na hivi karibuni katika kila Kijiji,  TANESCO watasambaza nguzo 40 kupeleka umeme maeneo ambayo bado.

Kuhusu Maji katika Kijiji cha Saydoda na Vijiji vingine katika tarafa hiyo ya Bashnet, amesema wananchi watarajie huduma ya maji safi na salama wakati wowote kwani mkandarasi tayari yupo Kazini baada ya Serikali kutoa zaidi ya shilingi bilioni 5 kutekeleza Mradi mkubwa wa maji wa ziwa Madunga.

Akijibu Swali la Mwananchi kuhusu ukarabati wa miundombinu ya barabara za kata kwa kata na wilaya kwa wilaya, Meneja wa Wakala wa barabara za mjini na vijijini TARURA wilaya ya Babati Mhandisi Aloyce Nombo  amesema Serikali imeshatoa fedha na wakati wowote kazi inaanza kabla msimu wa mvua haujaanza.

Mhe.Sillo akiambatana na Wataalamu anaendelea na ziara za kijiji kwa Kijiji kuwasikiliza Wananchi na kuwaeleza mambo mbalimbali yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na serikali, baada ya  kumaliza kuzunguka kata kwa kata katika Jimbo hilo lenye kata 25.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi