Na John Walter -Arusha
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Vita Rashid Kawawa imefanya ziara katika Gereza la Karatu pamoja na kukagua miradi mbalimbali inayoendelea katika Gereza hilo ikiwemo ujenzi wa Mabweni Mawili ya Wafungwa pamoja na nyumba ya Mkuu wa Gereza ambayo ujenzi wake upo katika hatua ya msingi
Akizungumza katika kikao mara baada ya ziara hiyo iliyofanyika kwenye Gereza la Karatu mkoani Arusha leo Novemba 9, 2024 Mheshimiwa Kawawa alipongeza uongozi wa Gereza hilo kwa miradi inayoendelea pamoja na mazingira mazuri ya wafungwa na Mahabusu katika Gereza hilo
Aidha, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo alisema kuwa sambamba na utekelezaji wa Miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa, Gereza hilo litaanza kutumia nishati safi kwa ajili ya kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu ili kuachana na matumizi ya kuni kama ilivyoelekezwa na Serikali ambapo Gereza hilo lilipangiwa kuwa na aina mbili za Nishati ambazo ni nishati ya gesi iliyokandamizwa ( Liquid Petroleum Gas - LPG) na Mkaa wa Rafiki Briquettes


Mhe. Sillo aliongeza kuwa tayari yameshapokelewa majiko na vyungu kwaajili ya nishati ya Gesi iliyokandamizwa na eneo kwa ajili ya kuhifadhi mitungi ya gesi hiyo imeanza kujengwa, Mhe Sillo alisema kuwa kazi hiyo itakamilika ndani ya siku kumi kuanzia Novemba 9, 2024
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza CGP Jeremiah Katungu aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha huduma mbalimbali za Magereza ikiwemo matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia chakula cha Wafunguwa ambapo alisema hatua hiyo itapunguza gharama na uchafuzi wa mazingira

