Tanga Yazindua Kampeni ya Usafi “Balozi Dkt. Batilda Mazingira Day”

 


Na Rebeca Duwe, Tanga


Serikali ya Mkoa wa Tanga imezindua kampeni maalum ya usafi na utunzaji wa mazingira ijulikanayo kama “Balozi Dkt. Batilda Mazingira Day”, ambayo itakuwa ikifanyika kila Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi.



Kampeni hiyo inalenga kuhakikisha kila mwananchi anawajibika kusafisha na kutunza mazingira katika maeneo yake ya kazi na makazi, huku akiepuka tabia ya kutupa taka ovyo.


Kikosi maalum kuhamasisha usafi

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, alisema Serikali imeona umuhimu wa kuimarisha usafi na utunzaji wa mazingira katika maeneo yote ya mkoa.



Alisema Serikali imeunda kikosi kazi maalum kitakachokuwa na jukumu la kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kuhamasisha utunzaji wa mazingira kuanzia ngazi ya mitaa hadi vijiji.


Aidha, kikosi hicho kitafuatilia utekelezaji wa sheria ndogo za mazingira na kuwachukulia hatua watu watakaobainika kutupa taka ovyo.


Kwa mujibu wa Dkt. Burian, watakaokiuka sheria hizo wanaweza kukabiliwa na faini ya kuanzia Shilingi 50,000, kulingana na sheria ndogo za mazingira za Halmashauri husika.


“Tutakuwa na kamati ya ukaguzi itakayohusika na kubaini changamoto, kutoa elimu na maelekezo. Pale sheria itakapokiukwa na mhusika akaonekana anaendelea kukaidi, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa miongozo,” alisema Dkt. Burian.


Vijana 50 kushiriki katika utekelezaji

Dkt. Burian alisema kikosi hicho kinaundwa na vijana 50 ambao, pamoja na kutekeleza sheria ndogo za mazingira, watakuwa wakikusanya taarifa kuhusu maeneo yanayohitaji usafi.


Taarifa hizo zitawasilishwa kwenye Halmashauri husika kwa ajili ya kuchukua hatua, ikiwemo kupeleka magari ya kukusanya na kuondoa taka.


Alisisitiza kuwa lengo la Serikali si kukusanya faini kutoka kwa wananchi, bali kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama.


“Timu hii haitakuwa juu ya sheria. Watakula kiapo kwamba hawatapokea rushwa wala kutumia nguvu wakati wa kuwakamata wanaokiuka sheria. Tozo zote zitakazokusanywa kisheria zitafanyika kupitia POS na risiti zitatolewa,” alisisitiza.


NEMC kushirikiana na Halmashauri

Kwa upande mwingine, Dkt. Burian alisema kikosi hicho kitashirikiana na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Halmashauri ya Jiji la Tanga katika kuhakikisha sheria za mazingira zinatekelezwa.


Alisema hatua hiyo inalenga kuweka mfumo rasmi wa kushughulikia ukiukwaji wa sheria za mazingira, huku makusanyo yote ya faini yakiingizwa katika mfumo rasmi wa ukusanyaji wa mapato.


Mkuu huyo wa Mkoa pia amezitaka Halmashauri zote 11 zilizopo Mkoa wa Tanga, chini ya usimamizi wa Wakuu wa Wilaya, kuhakikisha kampeni hiyo inatekelezwa katika maeneo yao.


Aliwataka wananchi kushiriki kwa hiari katika zoezi hilo la usafi ambalo litafanyika kila Jumamosi ya kwanza ya mwezi.


Tanga yatajwa kuchangia Sh bilioni 6 kwa mwezi

Dkt. Burian alisema Mkoa wa Tanga unachangia takribani Shilingi bilioni 6 kwa mwezi katika pato la Taifa, na kwamba mkoa huo unashika nafasi ya sita kati ya mikoa ya Tanzania.


Alisema mafanikio hayo yanapaswa kwenda sambamba na juhudi za kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa safi kuanzia ngazi ya kaya hadi maeneo ya biashara na huduma za umma.


NEMC: Kila mwananchi ana wajibu wa kutunza mazingira

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Meneja wa NEMC Kanda ya Bagamoyo, Ndimbumi Mboneke, alisema kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanayomzunguka yanakuwa safi na salama wakati wote.


Pia aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo vya uharibifu wa mazingira.


“Sheria ya mazingira imetoa haki kwa kila Mtanzania kuishi katika mazingira safi na salama, lakini pia imetoa wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama na kutoa taarifa anapoona kuna uharibifu wowote,” alisema Mboneke.


Katika uzinduzi huo, NEMC ilimkabidhi Mohamed Hilal cheti maalum cha shukrani kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha na kushiriki katika shughuli mbalimbali za utunzaji wa mazingira.


Meya wa Tanga: Maagizo ni amri, si ombi

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mustafa Seleboss, alisema Halmashauri iko tayari kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa katika kuhakikisha jiji linakuwa safi.


Seleboss alisema moja ya hatua zitakazochukuliwa ni kuendelea kupanga upya maeneo ya biashara, ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga katika maeneo yasiyoruhusiwa, hususan katikati ya stendi ya daladala.


“Hili zoezi tumelipokea kama wananchi wa Jiji la Tanga. Yale yote uliyoyaelekeza kwetu sisi ni amri, si ombi. Jina lako tutalienzi; kila itakapofika Jumamosi ya kwanza ya mwezi tutafanya usafi maalum,” alisema Seleboss.


Aliongeza kuwa Halmashauri itachukua hatua za kuondoa vibanda na vitu vinavyosababisha uchafu katika maeneo ya stendi, pamoja na kuondoa mawe yanayotumiwa na baadhi ya wafanyabiashara kuweka mizigo.


“Balozi Dkt. Batilda Mazingira Day” kuendelea kila mwezi

Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika jijini Tanga, ambapo Mkuu wa Mkoa, viongozi wa Halmashauri, NEMC na wananchi walishiriki katika zoezi la usafi katika eneo la Stendi ya Daladala Barabara ya 12.


Kampeni ya “Balozi Dkt. Batilda Mazingira Day” inatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi za Mkoa wa Tanga kuhamasisha wananchi kuchukua jukumu la pamoja katika usafi na utunzaji wa mazingira.


Serikali ya Mkoa imewataka wananchi, taasisi, wafanyabiashara na viongozi kushiriki katika kampeni hiyo ili kuhakikisha maeneo ya makazi, biashara na huduma za umma yanakuwa safi, salama na yanayolindwa dhidi ya uchafuzi wa mazingira.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi