Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' kuhakikisha huduma za kujifungua kwa akina mama zinaanza rasmi Desemba 24, 2024.
Pia Sendiga ameweka muda wa mwisho, Desemba 30, 2024, kwa ujenzi wa kituo hicho kukamilika ili wananchi waanze kunufaika na huduma bora za afya.
Sendiga ametoa maelekezo hayo alipofanya ziara ya kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Gisambalang, kilichopo wilayani Hanang', Desemba 16,2024 ambacho kimeendelea kuwa gumzo kutokana na changamoto za ukamilishaji wa ujenzi wake licha ya kupokea shilingi milioni 500 kutoka Serikalini.

Mradi huo ulioanza mwaka 2021 unalenga kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa vijiji vya Gisambalang, Waranga, Waama, na Masusu.

Hadi sasa jengo la huduma za wagonjwa wa nje(OPD) ndo linatoa huduma, lakini majengo ya maabara na wodi ya mama na mtoto bado hayajakamilika.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameitaka TAKUKURU kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matumizi ya shilingi milioni 500 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, akisisitiza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuboresha huduma za mama na mtoto nchini kote hivyo ni furaha yake kuona huduma hizo zinapatikana.
Mradi wa Kituo cha Afya cha Gisambalang ni muhimu kwa kuwa utaondoa kero za huduma za tiba kwa wakazi wa eneo hilo na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, hususan kwa mama na mtoto.
Wananchi wanasubiri kwa hamu kukamilika kwa mradi huo muhimu wapumzike kwenda umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
