Na John Walter-Hanang’
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mlima Hanang’,
Abubakar Mpapa, amesema juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika ndani ya
hifadhi hiyo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii wa ikolojia.
Akizungumza na Muungwana Blog, Mpapa
amesema moja ya kazi kubwa inayofanyika kwa sasa ni usafi wa mipaka ya hifadhi
hiyo kwa kuweka alama maalum.
Hatua hiyo inalenga kuzuia uvamizi,
migogoro kati ya hifadhi na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani, pamoja na
kuzuia majanga ya moto ambayo yamekuwa yakihatarisha mazingira ya mlima huo.
Aidha, amebainisha kuwa maafisa wa hifadhi
hiyo wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika mikutano ya kijamii kwa ajili ya
kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulinda na kuhifadhi Mlima Hanang’, ambao ni
hazina ya kiikolojia, kitamaduni na kiutalii kwa mkoa wa Manyara na taifa kwa
ujumla.
“Tunawahusisha wananchi kwa karibu kupitia
mikutano ya vijiji, ili waelewe thamani ya hifadhi hii na kushiriki katika
kuitunza,” alisema Mpapa.
Mlima Hanang’ umeendelea kuvutia wageni
kutoka ndani na nje ya nchi wanaofika kupanda mlima huo na kushuhudia mandhari
ya kuvutia.
Ndani ya hifadhi hiyo kuna ndege wa aina
mbalimbali, maporomoko ya maji ya asili, maeneo ya kimila ya kabila la
Wabarbaig kwa ajili ya ibada, na vivutio vingine vya kiutamaduni na kiikolojia.
Mbali na utalii wa kupanda mlima, shughuli
za ufugaji nyuki pia zinafanyika kwa kibali maalum, ambapo jamii inayozunguka
hifadhi hiyo imepewa fursa hiyo kwa lengo la kuinua kipato chao huku
wakishiriki kwenye uhifadhi wa mazingira.
“Kuna maeneo maalum ya kupumzikia ambayo
tumeyaandaa kwa ajili ya wageni wanaotembelea hifadhi hii, na tunaendelea
kuboresha huduma hizo ili kuvutia watalii wengi zaidi,” aliongeza Mpapa.
Katika hatua nyingine, Mhifadhi huyo
amesema serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za wageni pamoja na
uboreshaji wa miundombinu muhimu kama vile vyoo, mahema ya kulala, majiko kwa
ajili ya kupikia na njia za kupitika ndani ya hifadhi hiyo.
Maboresho hayo yamechangia kwa kiasi
kikubwa ongezeko la idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi ya Mlima Hanang’,
ambapo kwa sasa takribani watalii 3,000 hadi 5,000 huitembelea kila mwaka.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kuthamini sekta ya utalii na kutupatia fedha za maboresho, matokeo
yake yanaonekana wazi kwa ongezeko la watalii na hamasa kubwa ya wananchi
kushiriki kwenye shughuli za uhifadhi,” alisema Mpapa kwa furaha.
Mlima Hanang’ unaendelea kuwa mfano bora
wa hifadhi inayotunzwa kwa kushirikisha jamii, kukuza utalii wa ndani, na
kuimarisha uchumi wa wakazi wa eneo hilo kwa njia endelevu.
0 Comments