Na John Walter-Babati
Halmashauri ya mji wa Babati inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu waliobobea katika elimu jumuishi kwa watoto wenye mahitaji maalum, hali inayotishia ufanisi wa utekelezaji wa sera ya elimu jumuishi.
Kwa mujibu wa utafiti wa Marafiki wa Elimu Babati, kati ya walimu 328 waliopo katika shule 20 zilizofanyiwa tathmini – zikiwemo shule tano za sekondari na 15 za msingi – ni walimu saba pekee waliofunzwa mahususi kufundisha watoto wenye mahitaji maalum.
Mratibu wa Marafiki wa Elimu Babati, Gaudensia Igoshalimo, amesema hali hiyo inawanyima watoto wenye ulemavu nafasi ya kupata msaada stahiki katika mazingira ya kawaida ya shule.
“Watoto hawa wanahitaji msaada maalum kutoka kwa walimu waliobobea, lakini uhaba huo unaathiri maendeleo yao ya kitaaluma,” alisema Igoshalimo.
Makamu Mwenyekiti wa Marafiki wa Elimu, Frank Mollel, aliongeza kuwa changamoto hiyo si kikwazo kwa wanafunzi pekee bali pia kwa walimu wasiokuwa na mafunzo ya kina ya elimu jumuishi.
“Walimu wa kawaida wanajitahidi, lakini wanahitaji mafunzo maalum ili kuwahudumia ipasavyo,” alisema Mollel.
Mbali na uhaba wa walimu, utafiti huo umebaini kuwa shule nyingi hazina miundombinu rafiki kwa watoto wenye ulemavu, ikiwemo ngazi zisizo na vikwazo, vyoo maalum na njia za kupita kwa wanaotumia viti mwendo.
Yahaya Mpungi, Mjumbe wa Bodi ya Shule ya Msingi Bonga, amesema jamii haijaweka mkazo wa kutosha kuhakikisha mazingira ya shule yanakuwa shirikishi.
Wadau kama Suzana Mushi na Sweetbert Wamalwa, wameitaka serikali na washirika wa maendeleo kuwekeza zaidi kwenye miundombinu na mafunzo ya walimu ili kufanikisha elimu jumuishi.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Babati, Simon Mumbee, amesema serikali imelipokea suala hilo na tayari ina mipango ya kuongeza walimu wa elimu maalum na kuboresha miundombinu.
“Tumejipanga kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa elimu kwa sababu ya ulemavu,” alisema Mumbee.
Afisa Elimu Sekondari wa mji wa Babati, Paschalina Lowokelo, ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa suluhu.
Kwa mujibu wa utafiti, Halmashauri ya mji wa Babati ina watoto 113 wenye ulemavu waliopo shule mbalimbali, lakini ni shule moja tu – Shule ya Msingi Kwaang’ – inayopokea ruzuku ya wanafunzi wenye ulemavu na Hata hivyo, pia inakabiliwa na uhaba wa vifaa kama viti mwendo na magongo.
Mwakilishi wa shirika la Haki Elimu, Rose Kalage, alisema ufuatiliaji huo unafanyika katika wilaya tano – Geita, Ukerewe, Tabora, Babati na Mpwapwa – ili kuongeza hamasa na kuboresha utekelezaji wa elimu jumuishi.
Wadau walishauri serikali inapopanga bajeti kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum izingatie pia vifaa kama fimbo nyeupe, magongo, viti mwendo na vilevile kuwatambua watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya mji wa Babati Ali Kombo, amewataka maafisa wa kata kuwatambua watoto wenye ulemavu ili wapate haki yao ya msingi ya elimu.
Kikao hicho cha Marafiki wa Elimu, kilichofanyika mjini Babati, kiliwahusisha maafisa elimu, maafisa maendeleo ya jamii, wadau wa elimu na Mkurugenzi wa mji wa Babati, kikilenga kutoa mrejesho wa ufuatiliaji wa mkakati wa taifa wa elimu jumuishi na kuhimiza maboresho ya utekelezaji wake.
Chini hapa ni picha mbalimbali wakati wa mkutano huo.
0 Comments