Na John Walter-Babati, Manyara
Jeshi la Polisi mkoani Manyara linamshikilia mwanaume mmoja aitwaye Christopha Boay (60), mkazi wa kijiji cha Mgugu wilayani Babati, kwa tuhuma za kumuua kwa kikatili mwanamke anayefahamika kwa jina la Clarah Bonifasi (26) kwa kumkata kata kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake mbele ya watoto wake wadogo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, likiwemo Stella Mohamed, ambaye naye alijeruhiwa na mtuhumiwa wakati wa jaribio la kumzuia, wanasema walishangazwa na tukio hilo kwani Boay alikuwa anaheshimika kijijini na hakuwa na matatizo yoyote yaliyowahi kuripotiwa tangu aanze kuishi eneo hilo miaka mitatu iliyopita.
“Tulikuwa tunamuheshimu sana, ni mzee mkubwa, hakuwahi kuonesha tabia mbaya, alikuwa anaishi kwa amani na majirani wote, Mwanamke aliyemuua alikuwa akimuita Baba kwa heshima tu ya utu uzima wake,” alisema mmoja wa mashuhuda.
Inaelezwa kuwa marehemu Clarah Bonifasi alikuwa akiishi chumba cha nyuma cha nyumba moja na mtuhumiwa, pamoja na watoto wake wawili, huku Boay akiishi upande wa mbele.
Hakukuwa na mgogoro wowote uliowahi kuonekana baina yao, na majirani walithibitisha kuwa waliishi kwa maelewano na heshima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Magugu, Lohay Amos, amelilaani vikali tukio hilo akisema limetokea Julai 1,2025 majira ya saa tatu asubuhi katika kitongoji cha Mbugani, na kuongeza kuwa tukio hilo limeishtua jamii nzima ya kijiji hicho.
“Mara nyingi matukio kama haya yanahusiana na wivu wa mapenzi, lakini kwa hili bado haijajulikana sababu hasa, na tunasubiri uchunguzi wa vyombo vya dola,” alisema Lohay.
Mwenyekiti amewataka wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo la kusikitisha.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo cha afya Magugu kwa uchunguzi wa kitabibu, huku watoto wa marehemu ambao walishuhudia tukio hilo wakichukuliwa na majirani.
0 Comments