Na John Walter-Simanjiro
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, ameweka jiwe la msingi kwenye jengo la Soko la Madini (Tanzanite Trading Centre) lililopo Mirerani na kumtaka mkandarasi, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha ujenzi huo unakamilika mapema kabla ya mwisho wa mwezi huu.
RC Sendiga amesema hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 98 na hakuna sababu ya kuchelewesha kukamilika kwake, hasa ikizingatiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tayari ametoa zaidi ya shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya mradi huo.
Aidha, RC Sendiga amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kuhakikisha maboresho ya mazingira ya ndani na nje ya eneo hilo yanakamilika haraka, ili ifikapo Septemba 15, 2025, shughuli rasmi za uuzaji na uchakataji wa madini zianze katika soko hilo.
Vile vile, ameelekeza viwanja vinavyozunguka eneo la soko vitolewe kwa wafanyabiashara bila urasimu, ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Mirerani.
“Viwanja ni mali yetu sisi wananchi wa Mirerani, nataka utolewaji wake uwe wazi, tusifanye urasimu, ili wananchi wanufaike moja kwa moja na uwekezaji huu mkubwa,” alisema RC Sendiga.
Ameongeza kuwa uwepo wa soko hilo utaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Mirerani na Wilaya ya Simanjiro kwa ujumla, sambamba na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia biashara ya madini ya Tanzanite.
Pamoja na hayo, Sendiga amewataka wakazi wa Mirerani na Simanjiro kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Picha mbalimbali wakati wa uwekaji jiwe la msingi.









