Na John Walter-Babati
Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) imetoa shukrani kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (WMJJWMM) kwa tuzo na vyeti vya heshima ilivyokabidhiwa kwa uongozi na wanachama wake tarehe 26 Agosti 2025.
Mwenyekiti wa Taifa wa SMAUJATA, Sospeter Mosewe Bulugu, amesema wizara hiyo chini ya Waziri Dkt. Dorothy Gwajima na Katibu Mkuu wake, Dkt. John Jingu, imeonesha kuthamini mchango wa SMAUJATA katika shughuli za maendeleo ya jamii, ustawi wa familia na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto.
“Kwa niaba ya SMAUJATA nawapongeza kwa tuzo hizi ambazo si tu ni heshima kwetu, bali ni chachu ya kuongeza nguvu na morali katika kujitolea zaidi kwa jamii. Tunatambua mchango wa kila Shujaa mmoja mmoja ndani ya jumuiya, kwani kila mmoja ameweka jasho lake katika kufanikisha mafanikio haya,” alisema Bulugu.
Aliongeza kuwa SMAUJATA imekuwa ikishirikiana na wizara husika katika utekelezaji wa afua za ustawi wa jamii ikiwemo uanzishwaji wa madawati ya jinsia ndani na nje ya shule, ushiriki katika kamati za ulinzi na usalama wa mtoto mtandaoni pamoja na mpango wa MTAKUWWA I na II.
Aidha, Bulugu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake na ushirikiano kupitia watendaji wa serikali katika ngazi zote, wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia na watoto.
“Tuzo hizi kwetu ni deni la imani kwa Taifa letu na Rais wake. Tunaahidi kuendelea kuchapa kazi tukizingatia sheria za nchi na maelekezo ya taasisi zinazotusimamia,” alisisitiza Bulugu.
0 Comments