Na John Walter-Babati
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Manyara
limeguswa na maisha ya mama mmoja mkazi wa Mtaa wa Block X, Babati, ambaye kwa
zaidi ya miaka minane amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya Kisukari.
Asia Omari, mama wa watoto wawili, anasema ugonjwa
huo umemfanya awe tegemezi kwa binti yake Mariam, mwanafunzi wa kidato cha
kwanza, ambaye humchoma sindano asubuhi na jioni kila siku pamoja na kumhudumia
yeye na mdogo wake.
Kutokana na changamoto za kifamilia, Mariam mara
nyingine hulazimika kuacha masomo ili kutafuta riziki ya kuwahudumia mama na
mdogo wake.
Familia hiyo haina makazi ya kudumu na kwa sasa
wanaishi katika nyumba ya msamaria mwema baada ya baba yao kuwakimbia muda
mrefu.
Baada ya taarifa za maisha ya Asia kuripotiwa na
waandishi wa habari, wadau mbalimbali wameguswa, wakiwemo wafanyakazi wa
TANESCO mkoa wa Manyara wakiongozwa na Afisa Uhusiano wa mkoa, Samwel Mandari.
Kwa pamoja walijitolea na kumkabidhi msaada wa
mahitaji mbalimbali ikiwemo kitanda na godoro, kwani awali walikuwa wakilala
chini.
Mandari ametoa wito kwa jamii kuendeleza moyo wa
kujitolea na kusaidia watu wenye mahitaji maalum, huku akisisitiza mshikamano
wa kijamii.
Akizungumza kwa hisia, Asia Omari ameshukuru msaada
huo na kuwaombea wafanyakazi wa TANESCO baraka kutoka kwa Mungu. “Msaada huu
umenipunguzia mateso, Mungu awabariki,” alisema.
Kwa upande wake, Mariam amesema anasikitika kumuona
mama yake akiteseka na ndoto yake kubwa ni kusoma kwa bidii ili kuwa daktari,
ili siku moja aweze kumtibu.
Asia anaeleza kuwa mara nyingi hupata maumivu makali
mwili mzima na miguu kufa ganzi, hali inayomlazimu kuhudhuria kliniki kila
Alhamisi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, lakini mara nyingi hana
hata nauli ya kwenda na kurudi.
Picha mbalimbali wakati wa zoezi la utoaji msaada.
0 Comments