Na John Walter-Kiteto
Wakili Edward Ole Lekaita, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kiteto aliyemaliza muda wake, ameibuka mshindi kwa kishindo katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuwania tena ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika matokeo rasmi yaliyotangazwa, Ole Lekaita amezoa kura 12,532, akimuacha kwa mbali mshindani wake wa karibu Sisca Seuta aliyepata kura 1,919, akifuatiwa na Boniface Hindi Edward aliyepata kura 1,294, huku Alais Nangoro akijizolea kura 753 pekee.
Ushindi huu mkubwa kwa Ole Lekaita unaashiria kuungwa mkono kwa kiwango kikubwa na wajumbe wa CCM wilayani Kiteto, hali inayoashiria kurejea kwake katika kinyang’anyiro cha ubunge kwa mara nyingine.
Wakili Ole Lekaita amewahi kutumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha nyuma ambapo alijizolea sifa kwa utetezi wa masuala ya wananchi na kushiriki kikamilifu katika mijadala ya bunge.
Kwa sasa macho yote yanaelekezwa kwenye hatua inayofuata ya uteuzi ndani ya chama na hatimaye uchaguzi mkuu, ambapo atakabiliana na wagombea wa vyama vingine iwapo atateuliwa rasmi kupeperusha bendera ya CCM.
0 Comments