F Mwili wa mwanamke wakutwa mtoni ukiwa mtupu. | Muungwana BLOG

Mwili wa mwanamke wakutwa mtoni ukiwa mtupu.


Na John Walter-Mbulu

Mkazi wa kitongoji Cha  Qatajiting, kijiji cha Tumati, wilayani Mbulu mkoani Manyara, Bi Rosemary Godfrey Chaula (30), ameaga dunia kwa tukio la kikatili baada ya kudaiwa kubakwa na kuuawa na watu wasiojulikana, kisha mwili wake kutupwa mtoni kijijini hapo.

Kwa mujibu wa taarifa ya familia iliyosomwa katika historia ya marehemu, Rosemary aliondoka nyumbani kwake tarehe 27 Agosti 2025, majira ya saa 11 jioni, lakini hakurudi. 

Siku iliyofuata, 28 Agosti 2025, mwili wake ulipatikana mtoni ukiwa mtupu. Marehemu ameacha watoto wawili.

Septemba 1,2025, mamia ya waombolezaji wamehudhuria mazishi ya marehemu kijijini Tumati, akiwemo Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Kaskazini, Shujaa Ezekiel Tlanka, ambaye alikemea kitendo hicho cha kinyama.

Tlanka ameliomba jeshi la polisi na vyombo husika kuhakikisha wahusika wanapatikana na kuchukuliwa hatua kali za kisheria. 

Aidha, ameitaka jamii kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola  ili kukomesha matukio ya aina hiyo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Qatajiting kulikotokea tukio hilo, Zakaria Damiano, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu sita wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano kuhusu tuhuma hizo.

Mazishi hayo yameacha simanzi kubwa kijijini, huku familia na wananchi wakitoa wito wa kuimarishwa kwa ulinzi na usalama wa wanawake na watoto katika maeneo ya vijijini.

Post a Comment

0 Comments