F Bilioni 1.5 kutumika kujenga daraja la kinambichi babati | Muungwana BLOG

Bilioni 1.5 kutumika kujenga daraja la kinambichi babati


Na John Walter-Babati

Serikali imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Kinambichi katika mwaka wa fedha 2026, hatua inayolenga kuboresha mawasiliano na kurahisisha usafiri kwa wananchi wa vijiji vya Gichameda na Magugu wilayani Babati.

Akizungumza wakati akiwasilisha bajeti kwenye Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Babati, Mhandisi Aloyce Nombo amesema daraja hilo lililopo kitongoji cha Kinambichi lina umuhimu mkubwa katika kuunganisha mawasiliano ya vijiji hivyo, hususan kipindi cha mvua ambapo usafiri hukumbwa na changamoto.

Awali, Diwani wa Kata ya Magugu Stanley Charles alihoji kuhusu mpango wa ujenzi wa daraja hilo na kupatiwa ufafanuzi kuwa tayari fedha zimetengwa huku maandalizi ya utekelezaji yakiwa yanaendelea.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Nombo amesema bajeti ya TARURA Babati kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ni shilingi bilioni tatu, milioni themanini na tano na elfu themanini (3,085,080,000), fedha zitakazotumika katika ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja wilayani humo.

Aidha, mradi wa barabara ya Magara Maji Moto kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara umetengewa shilingi milioni 426, ambapo taratibu za mwisho zinaendelea kukamilishwa kwa kushirikiana na World Bank ili kuruhusu utekelezaji wa mradi huo kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

Ujenzi wa miradi hiyo unatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao, kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii pamoja na kukuza shughuli za utalii na biashara katika wilaya ya Babati.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni