Na John Walter-Manyara
Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme
katika vitongoji 267 vya mkoa wa Manyara kwa gharama ya shilingi bilioni 45.8
kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Akizungumza wakati wa hafla ya kumtambulisha mkandarasi
atakayetekeleza mradi huo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi
Herini Mhina, amesema mkataba wa utekelezaji wa mradi huo ni wa kipindi cha
miaka mitatu na utatekelezwa katika halmashauri zote za mkoa wa Manyara.
Mhandisi Mhina amesema mradi huo unalenga kuongeza
upatikanaji wa umeme vijijini, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii,
pamoja na kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na biashara ndogondogo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga,
amewaagiza wakuu wa wilaya zote za mkoa huo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa
mkandarasi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati
uliopangwa. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuwa mradi
huo hauna fidia, hivyo wanapaswa kushirikiana kwa dhati bila kuweka vikwazo.
Naye mkandarasi aliyekabidhiwa utekelezaji wa mradi huo,
Patrick Mong, amesema wana lengo la kukamilisha mradi huo ndani ya miezi 33.
Ameongeza kuwa maandalizi yote yamekamilika na kazi za utekelezaji zinaanza
rasmi tarehe 9 Februari mwaka huu.
Mradi huo unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na
kijamii kwa wananchi wa mkoa wa Manyara kwa kuongeza fursa za ajira, uwekezaji
na maendeleo endelevu.

0 Maoni