Na John Walter-Babati
Wakazi wa mitaa ya Mruki na Msasani katika Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani
Manyara wameiomba serikali kuwajengea daraja la kudumu katika Mto Fahhay ili
kuondoa hatari inayowakabili wanafunzi wa Shule ya Msingi Mruki wanaolazimika
kuvuka daraja la mbao kila siku wanapoenda shuleni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamesema daraja
hilo la muda limekuwa likitumika kwa zaidi ya miaka mitatu, lakini kwa sasa
limeanza kuwa hatari kutokana na baadhi ya mbao na miti iliyotumika kulijenga
kuoza na idadi ya watumiaji kuongezeka.
Shule shikizi ya Msingi Mruki yenye takribani wanafunzi 200
ilianzishwa na Halmashauri ya Mji wa Babati kwa lengo la kupunguza umbali mrefu
waliokuwa wakitembea wanafunzi kutoka mitaa ya Mruki na Msasani kwenda katika
shule mama ya Msingi Msasani na Darajani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi Mruki, Bakari Said,
amesema licha ya daraja hilo kuwa mkombozi kwa wanafunzi kwa kipindi cha zaidi
ya miaka mitatu, sasa limekuwa tishio kwa usalama wao hasa wakati wa msimu wa
mvua.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mruki, Abdilahi
Rajabu, amesema daraja hilo ni kiungo muhimu kinachounganisha mitaa ya
Sinai na Mruki, ambapo asilimia kubwa ya watoto kutoka maeneo hayo husoma
katika shule hiyo shikizi ya Mruki.
Naye Mariam Hamis, mkazi wa Mruki, ameiomba serikali
kuharakisha ujenzi wa daraja la kudumu ili kuwaepusha watoto na wakazi wa eneo
hilo na hatari ya kuanguka mtoni wanapovuka.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Samia Issa
Ramadhani na Halima Idd wamesema hulazimika kuvuka daraja hilo kila
siku kwenda na kurudi shuleni, hali inayowatia hofu hasa wakati daraja
linapokuwa na utelezi au kuharibika.
Aidha, Agostino Balohho, ambaye ni mlinzi wa Shule ya
Msingi Mruki, amesema daraja hilo la mbao ni njia fupi inayotumiwa na wanafunzi
kutoka Mtaa wa Sinai kufika shuleni na pia hutumiwa na wakazi wa Mruki kama
njia ya mkato kwenda mjini Babati kufuata huduma mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo, wakazi hao wameiomba serikali pamoja
na wadau wa maendeleo kuwasaidia kujenga daraja la kudumu litakalohakikisha
usalama wa wanafunzi na wananchi wanaolitumia kila siku.

0 Maoni