NA REBECCA DUWE, TANGA
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mang’onda, amesema ameridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Zahanati ya Muungano iliyopo Kitongoji cha Machemba, Kata ya Mlingano, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Mang’onda alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi na ukaguzi wa zahanati hiyo, akieleza kuwa kazi iliyofanyika ni nzuri na inaleta matumaini kwa wananchi kama ambavyo Serikali imekusudia katika kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.
Aidha, aliwashukuru wadau wa maendeleo, hususan Islamic Help, kwa mchango wao katika ujenzi wa zahanati hiyo, akisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Awali, akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Dk. Fani Musa, alisema mradi huo upo katika Kijiji cha Muungano, Kata ya Mlingano, Tarafa ya Ngomeni, Wilaya ya Muheza.
Dk. Musa alisema mradi huo umejengwa kwa ufadhili wa Islamic Help na ulianza kutekelezwa Machi 2, 2025. Aliongeza kuwa jiwe la msingi liliwekwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi.
Alisema hadi kukamilika kwake, mradi huo umegharimu jumla ya shilingi milioni 165.9 za Kitanzania, ambapo sehemu ya fedha hizo ilitumika kwa ujenzi wa zahanati na nyingine kwa ununuzi wa vifaa tiba.
Kwa mujibu wa Dk. Musa, mradi huo ulikamilika Oktoba 10, 2025 na baadaye kupatiwa usajili na kibali cha kutoa huduma na Wizara ya Afya. Zahanati ilianza rasmi kutoa huduma Januari 2, 2026 na hadi sasa takribani wananchi 850 wamehudumiwa.
Aliongeza kuwa zahanati hiyo itanufaisha wakazi 6,258 wa Kijiji cha Muungano, wakiwemo wanaume 3,089 na wanawake 3,169, kwa kuwapatia huduma bora za afya karibu na maeneo yao.
Mwisho.
